Marais wa Iran na Uturuki wakosoa sera za vikwazo na mashinikizo.

Marais wa Iran na Uturuki wakosoa sera za vikwazo na mashinikizo
Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki zinapinga vikali sera za vikwazo, mashinikizo na uchukuaji maamuzi ya upande mmoja kwenye uhusiano wa kimataifa.


Rais Hassan Rouhani alisema hayo jana Jumamosi huko Dushanbe,  mji mkuu wa Tajikistan, alipoonana na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan pambizoni mwa Mkutano wa Tano wa Kongamano la Maingiliano na Hatua za Kujenga Imani Barani Asia (CICA) na kuongeza kuwa, Iran ina hamu ya kuimarisha uhusiano wake na Uturuki hususan katika nyuga za uchumi na biashara.
Amesema hatua kadhaa muhimu zimechukuliwa katika miaka ya hivi karibuni, kwa ajili ya kuboresha na kunyayua katika kiwango cha juu zaidi uhusiano na ushirikiano wa nchi mbili hizi. 
Dakta Rouhani ameashiria pia kuhusu kuimarishwa ushirikiano wa Tehran na Ankara katika masuala ya kieneo na kusema kuwa, "Ushirikiano wa kieneo wa Iran, Uturuki na Russia katika masuala mbalimbali ya kieneo kama vile mchakato wa Astana, kupambana na ugaidi na kurejesha uthabiti nchini Syria ni masuala muhimu ya kuimarisha amani na uthabiti katika eneo."
Kwa upande wake Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema uhusiano wa nchi yake na Iran ni wa karibu na unazidi kuimarika katika nyuga zote zenye maslahi ya pamoja.
Amesema Uturuki ina azma ya kuboresha zaidi uhusiano wake na Iran katika nyuga tofauti. Marais hao wawili wamekosoa vikali sera za vikwazo na uchukuaji wa hatua za upande mmoja kwenye uhusiano wa kimataifa.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Iran na Uturuki zinakabiliwa na vikwazo vya viwango tofauti kutoka kwa Marekani.

parstoday

Comments