Walimu Watakiwa kuwapeleka wanafunzi kwenye maonyesho.

Image may contain: 2 people, people smiling, people standingWAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amewataka walimu nchini kuwapeleka wanafunzi wao katika maonesho ya Nane nane ili waweze kujifunza kwa vitendo zaidi.
Akizungumza wakati alipofika katika maonesho hayo huko Dole, Mhe Riziki amesema kufanya hivyo kutaweza kuibua vipaji mbalimbali vya wanafunzi ambavyo vitawafanya kutambua nini wafanye kutokana na yale watakayojifunza kwa vitendo.
Amesema pamoja na kujifunza kwa wanafunzi hao pia watakuwa wametekeleza agizo la Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein la kutaka kupelekwa wanafunzi katika maonesho hayo kwa lengo la kujifunza.
Aidha amesema amefarajika sana kuona baadhi ya Wanafunzi na Walimu wao kufika katika maonesho hayo ambapo amewataka kuzingatia wanayoelimishwa pamoja na kuyafanyia kazi kwa vitendo wakiwa nyumbani, ili yaweze kuwasaidia katika maisha yao.
Aidha Mhe Riziki amesema maonesho ya mwaka huu yamefana kwa kiasi kikubwa ukilinganisha ya mwaka jana, kwani yameweza kushirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi pamoja na watu wenye ulemavu na kuweza kuonesha kazi zao pamoja na kutoa elimu juu ya kazi wanazozifanya, zikiwemo kilimo, ufugaji, kazi za mikono, kazi za amali na masuala ya kitaalamu.
Hata hivyo ameishauri Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuendelea kuzishirikisha Taasisi mbalimbali katika maonesho kama hayo hasa za Vyuo vya Amali na Vyuo vyengine, kwani watu wengi wanapata kujifunza kupitia maonesho kama hayo.
Pia amewashauri kuwashirikisha kwa wingi zaidi watu wenye ulemavu pamoja na Kupanga utaratibu maalumu wa kuwatembeza wageni wanaofika katika maonesho hayo ili kila mshiriki wa maonesho hayo aweze kutembelewa na kupata fursa ya kujitangaza.
"biashara itangazwayo ndiyo itokayo" amesitiza Mhe Riziki.Image may contain: 4 people, people standing, people sitting and indoor
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa maonesho hayo, wameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa ushirikiano wanaoutoa katika kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali ikiwemo Rushwa, Kilimo, pamoja na teknolojia mbalimbali nchini.
Baadhi ya Wananchi waliofika kuangalia na kujifunza katika maonesho hayo, wameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitalia Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kuweka maonesho kama hayo ambayo yamewapa fursa ya kujifunza masuala mbalimbali, ambapo wameshauri vipeperushi na majarida yanayotolewa katika maonesho hayo kuandikwa kwa lugha ya kiswahili ili kila mmoja aweze kujisomea na kuweza kuelimika zaidi.Image may contain: 3 people, people standing

Comments