Magaidi 20 waangamizwa na maafisa usalama kaskazini mwa Mali.

Magaidi 20 waangamizwa na maafisa usalama kaskazini mwa Mali
Kwa akali magaidi 20 wameuawa katika operesheni ya kutokomeza ugaidi inayojulikana kama 'Barkhane' huko kaskazini mashariki mwa Mali.


Taarifa ya Jeshi la Mali inasema kuwa, operesheni hiyo ya askari wa Mali ilifanyika jana Jumamosi kwa ushirikiano na wanajeshi wa Ufaransa katika kijiji cha Akabar eneo la Ménaka, kaskazini mashariki mwa nchi, ambapo magaidi 20 wameuawa.
Taarifa hiyo ya Jeshi la Mali hata hivyo haijatoa maelezo zaidi kuhusu operesheni hiyo.
Magenge yenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh yamekuwa yakiendeleza harakati na mashambulizi yao katika eneo hilo. 
Haya yanajiri siku chache baada ya makumi ya watu wakiwemo watoto wadogo kuuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia kijiji cha Sobane-Kou, katikati ya nchi hiyo. 
Katika hatua nyingine, watu 35 wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya silaha katika nchi nyingine ya Afrika Magharibi ya Nigeria.
Kwa mujibu duru za habari, watu waliokuwa wamebeba silaha wakiwa juu ya pikipiki wamewashambulia wakulima katika vijiji vya Kwallido, Tungar Kahau na Gidan Wawa katika jimbo la Zamfara kaskazini magharibi mwa nchi, ambapo 35 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
parstoday.

Comments