WIZARA
ya Elimu na Mafunzo ya Amali imetakiwa kuhakikisha kwamba katika mipango na
taratibu wanazoziandaa ni vyema wakajipanga vizuri ili uwepo mfumo bora na
endelevu wa uratibu na usimamizi wa shughuli za Skauti katika skuli za Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito huo katika maadhimisho ya miaka 107
ya Skauti Zanzibar yaliyofanyika katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar.
Katika
hotuba yake Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa ni muhimu uwepo mfumo wa namna moja
na unaotambulika rasmi katika kila ngazi inayohusika jambo ambalo litaongeza
hamasa na mipango katika kukuza uzalendo, kuamsha ari na kuwakumbusha
wananfunzi historia ya nchi yao.
Alieleza
kuwa miongoni mwa mambo ambayo yanahitaji kusimamiwa vyema ni lazima kuongezeka
kwa heshima, hadhi na thamani za nyimbo za Taifa, Wimbo wa Mashujaa, bendera na
nembo za Taifa.
Alisisitiza
kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inapaswa kuangalia kuona namna bora
ambayo misingi wanayopewa vijana wa Skauti wanakuzwa nayo ili wawe raia wema na
wazalendo.
Rais
Dk. Shein aliwataka viongozi wa vijana wa Skauti kuwa wamoja na kuepuka vitendo
vyovyote vyenye kuashiria ubaguzi kwani wao ni wamoja.
Aidha,
Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwaandaa vijana hao ili kuwa wazalendo wa Taifa,
akibainisha maendeleo ya nchi na jamii yoyote huletwa na wazalendo.
Alisema
uzalendo ndio unaohimiza mtu kufanya bidii, ari, hamasa na kuwa muadilifu
katika kazi za halali na hivyo kupata tija na manufaa.
Aliwapongeza vijana wa skauti kwa jinsi walivyo makini na wanaotunza nidhamu, akibainisha kuwa ndio msingi wa mafanikio ya kila kitu.

Comments