wananchi waaswa juu ya mafuriko.

Uwepo wa mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha maeneo mengi nchini, kwa upande wa visiwa vya  Zanzibar katika wilaya ya mjini zaidi ya nyumba 141 zimeathiriwa vibaya na mvua hizo na kusababisha wakaazi wake kuhama makaazi yao kwa lengo la kujinusuru na maafa zaidi.
Baadhi ya  maeneo yalioathiriwa na mvua hizo ni shehia ya Mwanakwerekwe mjini Unguja, Tomondo ,Ziwa Maboga, Ziwatuwe, Pangawe, Kinuni na baadhi ya maeneo mengine mbali mbali.
Baadhi ya wahanga wa kadhia hio wakizungumza na gazeti hili walisema wamelazimika kuhama kwa sababu ya uwepo wa mvua kubwa zaidi usiku.
Ali Abdalla Juma mkaazi wa Nyerere, alisema imemlazimu kuhama baada ya maji mengi kuingia kwenye nyumba yake kupitia sehemu mbali mbali  na kufanya nyumba hio kujaa maji.
Alisema kwa sababu ya mazingira hayo alilazimika kuhamisha baadhi ya vitu vyake ndani ya nyumba hio usiku wa manane na kusema bila ya kufanya hivyo huwenda madhara makubwa zaidi yangemtokea.
Farhat Zagu wa Tomondo, alisema hadi sasa bado hana sehemu maalumu ya kukaa badala yake imemlazimu kuomba sehemu ndogo kwa majirani zake kutokana na tatizo kama hilo ambalo limewakumba wengi.
Nae Mkuu wa Wilaya Mjini, Marina Joel Thomas, alisema ipo haja ya wananchi kuwa makini zaidi katika kipindi hichi na kuwataka kuhama katika maeneo yaliohatarishi na mvua hizo.
Alisema jamii inapaswa kujikinga na  athari hizo ambazo  zinaweza kuwa kubwa zaidi, iwapo wataendelea kubakia katika maeneo yote yalio hatarishi.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar, Muhidini Ali Muhidini, alisema kwa kiasi kikubwa wananchi wamehamasika kuhama kwenye maeneo hatarishi.
Alisema hali hio imediriki kutokana na elimu waliopatiwa kutoka katika Kamisheni hio ya kukabiliana na maafa na kwamba utaratibu huo utawanusuru wengi kuepuka na majanga zaidi na kuipunguzia mzigo Serikali ambao ungeweza kujitokeza.
Pamoja na hayo aliseka Kamisheni hio ipo karibu na wananchi zaidi katika kipindi hichi na imejiandaa na lolote lile ambalo litatokea.
Zanzibarleo.

Comments