Umashuhuri wa chama tawala cha ANC wapungua katika uchaguzi wa Afrika Kusini.

Umashuhuri wa chama tawala cha ANC wapungua katika uchaguzi wa Afrika Kusini
Matokeo yasiyo rasmi ya uchaguzi nchini Afrika Kusini yanaonyesha chama tawala cha Africa National Congress ANC kinaelekea kupata ushindi na kuendelea kusalia madarakani ingawa umashuri wake umepungua.


Matokeo yanaonyesha kuwa hata kama ANC kitapata ushindi, huu utakuwa uchaguzi wenye matokeo mabaya zaidi kwa chama hicho tokea kiingie madarakani mwaka 1994.
Taarifa zinasema hadi kufikia saa 12 asubuhi leo, asilimia 74 ya vituo vya kupigia kura vilikuwa vimetangaza matokeo ambapo chama cha ANC kimepata asilimia 57.17 ya viti vya bunge kikifuatwa na chama cha DA ambacho kina asilimia 21.87 na EFF kikishika nafasi ya tatu kwa asilimia 10.7.
Inatabiriwa kuwa ANC kitapata baina ya asilimia 55-60 ya viti vyote vya bunge na hivyo kutoa changamoto kubwa kwa chama hicho.
Chama hicho cha zamani cha ukombozi cha Nelson Mandela hakijawahi kupata chini ya asilimia 60 ya kura katika uchaguzi wa taifa tangu kilipoingia madarakani nchini Afrika Kusini kupitia uchaguzi wa kwanza uliowahusisha watu wote mwaka 1994.
Uchaguzi huu ndio changamoto ya  kwanza kubwa tangu Cyril Ramaphosa alipochukua nafasi ya rais wa nchi kutoka kwa Jacob Zuma, aliyekumbwa na kashfa kadhaa mnamo Februari 2018.
Katika uchaguzi uliopita mwaka 2014, chama cha ANC kilishinda asilimia 62 ya kura, chama cha DA kilipata asilimia 22 na EFF asilimia 6.
 parstoday.

Comments