
Akizungumza wakati alipozindua Vuguvugu la kuhamasisha malezi bora na matunzo ya familia, katika ukumbi wa Shekh Idrissa Abdul Wakil kikwajuni Mjini Unguja Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amesema mashirikiano mazuri pia yanapelekea kila mmoja kutimiza wajibu wake juu ya maalezi bora kwa watoto na kupata Taifa lenye watoto wenye maadili mema.
Amesema malezi mazuri kwa vizazi vyao ni chachu ya Taifa kwa kuwa na wasomi imara Kwani mabadiliko ya kimaendeleo katika nchi yanaenda sambamba na kuwa na watoto waliolelewa katika malezi bora.
"Kujenga ustawi mwema wa malezi ni suala lililosisitizwa katika vitabu vya dini zote Kwani kila mtu ni mchunga na ataulizwa juu ya alichokochunga" amesisitiza Mhe Riziki.
Aidha amewataka wazazi kumaliza changamoto za malezi Kwani hupelekea watoto kuingia katika majaribu na vishawishi vya mambo mabaya.
Amesema ni vyema wazazi kudumisha mila na desturi za mzanzibar na kufuatilia mienendo ya watoto kwani kutasaidia kumaliza vitendo vya udhalilishaji katika jamii.
Mhe Riziki amesema maadhimisho ya siku ya familia Duniani ni kuifanya jamii kutafakari juu ya matatizo yanayowakabili watoto Duniani.
Nae Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya kazi uwezeshaji,Wazee, Vijana, wanawake na watoto bi Mwanajuma Majid Abdalla amesema lengo la kuzindua vuguvugu Hilo ni kuzitaka familia kujua wajibu wao ili kupata kizazi chenye malezi bora na kutokomeza kabisa matendo ya udhalilishaji katika jamii.
Amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la watoto Duniani UNICEF wamezindua kampeni ya kutokomeza matendo yanayodhofisha malezi bora.
Nae Bi Mwanaisha makame kutoka wilaya ya magharibi A akisoma risala kwa niaba ya wazazi wenziwe wameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuandaa mikakati imara ya familia kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama.
Aidha amewataka wazazi wenziwe kuwa na muamko wa malezi bora na kuwasaidia watoto wao katika makuuzi yao.
Siku ya familia huadhimishwa kila ifikapo tarehe 15 Mei, ambapo kwa Zanzibar imeadhimishwa kwa kuzindua vuguvugu la kuhamasisha malezi bora na matunzo ya familia ambapo kauli mbiu ni "Tuimarishe malezi bora kuhifadhi watoto tuzungumze nao na tuwapende."







Comments