Kamanda wa ngazi za juu katika Harakati ya Jihad Islami ya Palestina ametoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa, harakati za mapambano ya Palestina zimepata uwezo mpya wa kukabiliana na Israel katika vita vijavyo.
Jamil Alyan, kamanda wa ngazi za juu wa Jihad Islami ameongeza kuwa, makundi ya mapambano ya Palestina yana uwezo mkubwa ambao utatumika wakati muafaka kuzuia malengo ya kujitanua ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kamanda huyo wa ngazi za juu wa Jihad Islami ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kulinda haki za watu wa Palestina hasa katika Ukanda wa Ghaza.
Jamil Alyan aidha amesema utawala wa Kizayuni ungali unaendeleza sera zake za ubeberu na kujitanua na kwa msingi huo hakuna matumaini yoyote ya kufikia mapatano na utawala huo.
Matamshi hayo ya Jamil Aylan yanakuja baada ya mapigano mapya baina ya makundi ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni kujiri kwa muda wa siku nne kuanzia Ijumaa iliyopita kufuatia hujuma ya utawala huo huko Ghaza. Katika mapigano hayo, Wapalestina 31 waliuawa shahidi na wengine 177 kujeruhiwa.
parstoday.
Comments