Ethiopia yawakamata watu 62 waliohusika na mapigano ya kikabila, wakimbizi warejea.


Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwakamata watu 62 ambao walihusika katika kuchochea mapigano ya kikabila hivi karibuni nchini humo.


Polisi katika mkoa wa Benishangul Gumuz uliopo magharibi mwa Ethiopia wamesema wamewakamata watu 62 wanaohusishwa na vurugu kali za kikabila.
Polisi wa Mkoa wa Benishangul Gumuz Mohammed Hamednil amesema watu hao 62 walikamatwa wakiwa na mamia ya silaha butu ambazo zinaaminika kwamba watuhumiwa hao walizitumia kwenye mashambulizi hayo ya kikabila. 
Mapigano hayo yanahusisha kabila la Gumuz na kabila la Amhara.
Habari zaidi zinasema serikali ya Ethiopia katika wiki za karibuni imewarejesha nyumbani wakimbizi wa ndani 875,000 waliokimbia mapigano ya kikabila na vurugu. 
Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Billene Seyoum, serikali pia inashughulikia kuwarejesha wakimbizi waliosalia na kuwafikisha mahakamani wale wanaohusika na msukosuko huo wa wakimbizi wa ndani.
Wakosoaji wa Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa nchi hiyo wanaamini kwamba marekebisho ya kisiasa aliyoyafanya ndiyo yameibua tena mapigano ya kikabila nchini humo.
parstoday.

Comments