RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein amefutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba na kuwataka kuendeleza amani na utulivu uliopo nchini ili maendeleo zaidi yazidi kupatikana.
Hafla hiyo ya futari iliyoandaliwa na Rais Dk. Shein kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba ilifanyika katika viwanja vya Ikulu ndogo Chake Chake, na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali, dini, vyama vya siasa pamoja na wananchi wa Mkoa huo.
Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Rais Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa huo Hemed Suleiman alieleza kuwa amani na utulivu ndio msingi wa maendeleo hivyo kila mmoja anapaswa kuilinda na kuiendeleza kwa nguvu zake zote.
Alisisitiza kuwa maendeleo yote yaliopatikana nchini yametokana na kuwepo kwa amani na utulivu mkubwa ambayo ndio chachu ya mafanikio hayo na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuyakuza maendeleo hayo kwa kadri uwezo utakapopatikana.
Alhaj Dk. Shein aliwatakia Ramadhani njema wananchi wa Mkoa huo na kuwasisitiza kuutukuza mwezi huo mtukufu kwa kusoma sana Qur-an kwani ndio mwezi ulioshuka kitabu hicho kitakatifu.
Alhaj Dk. Shein aliwataka wananchi wa Mkoa huo kuendelea kushirikiana na kupendana sambamba na kuwa wamoja huku akiwataka kuachama na mambo yote yaliyokatazwa ndani ya mwezi huu na miezi mengineyo ili waendelee kupata neema za Allah.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kupambana na vitendo na matukio yanayovunja maadili ya dini ya kiislamu na ambayo hayapaswi kufanyika katika jamii ukiwemo udhalilishaji wa wanawake na watoto pamoja na matumizi ya dawa za kulevya ambayo hayaleti taswira nzuri katika jamii.
Pia, Alhaj Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendelezwa na kudumishwa kwa usafi hasa katika kipindi hichi cha msimu wa mvua huku akieleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na athari za mvua kwa Unguja na Pemba.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwashukuru wananchi wote waliohudhuria katika futari hiyo aliyowaandalia na kupongeza jinsi walivyoonesha upendo mkubwa kwake wa kukubali muwaliko wake huo.
Comments