
Balozi Seif, aliyasema hayo wakati akijibu hoja za wajumbe wa baraza la wawakilishi waliopendekeza kwa serikali kuangalia uwezekano wa kujenga ofisi za kudumu majimboni za wajumbe wa baraza hilo.
Wajumbe hao walitoa pendekezo hilo katika kikao cha bazara la wawakilishi kinachofanyika Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Akijibu hoja hiyo Balozi Seif, alisema kwa muda mrefu zimejengwa ofisi za wabunge majimboni hawajui utendaji wa kazi zake kutokana na kutotumiwa vyema.
Balozi Seif alisema serikali itafanya utafiti ili iweze kupata njia muafaka itakayowezesha wajumbe hao kujengewa ofisi hizo.
Alisema wajumbe hao kuwa na ofisi za kudumu katika majimbo kutawawezesha kuwa karibu katika kuwahudumia wananchi sambamba na kuwasaidia katika maendeleo yao.
Alifahamisha, kabla ya ujenzi wa ofisi hizo, lazima serikali ijue mwenendo wa ufanyakazi kazi za ofisi za wabunge ambazo baadhi yao zipo mwituni na kushindwa kufanyia kazi zake ipasavyo.
“Tutafanya utafiti mwanzo kabla ya kujengwa ofisi za wawakilishi majimboni, tukithibitisha utendaji wa ofisi za wabunge, ndio tutaanza mchakato wa kujenga ofisi za wawakilishi”, alifahamisha Balozi Seif.
Hivyo alisema, iwapo serikali itajitosheleza juu ya utendaji kazi wa ofisi za wabunge majimboni, wataangalia kujenga za wawakilishi, ili ziweze kuwasaidia wananchi katika kupeleka kero zao kwa wakati na kutatuliwa changamoto zao.
Kuhusu mbadilishano wa majengo kati ya serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif alisema wamepeana kwa kuaminiana.
Alifahamisha, hivi sasa wapo katika mchakato wa upatikanaji wa hati za majengo hayo ambapo zoezi hilo linaendelea.
Zanzibarleo.
Comments