
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amesema Walimu Wakuu ndio wenye jukumu la kusimamia kazi kwa Walimu wengine ili kuleta maendeleo katika sekta ya Elimu nchini.
Akizungumza wakati akimtambulisha Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe Simai Mohamed Said kwa Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari za Unguja katika ukumbi wa Skuli ya Haille sselasie, amesema Kuna baadhi ya walimu wamekuwa wanaendelea kuwatoza pesa wanafunzi kwa visingizio mbalimbali hali ambayo Serikali ilipiga marufuku suala hilo.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haitowafumbia macho walimu wenye tabia hiyo na kuwataka walimu wakuu kuwafuatilia walimu hao ili kutimiza azma ya Serikali ya kutoa Elimu bure kwa wote.
Amesema pesa zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuhakikisha kuwa kila Mwanafunzi anapata haki yake ya Elimu bure kuanzia Maandalizi, Msingi hadi kidato cha nne kama inavoeleza sera ya Elimu ya mwaka 2006.
Aidha Mhe Riziki amesema Skuli zinaweza kuendeleza miradi ya uzalishaji mali ya Skuli na sio mwalimu kumchangisha mwanafunzi kwa malengo ya masomo.
Akizungumzia suala la kambi kwa Wanafunzi Mhe Riziki amewataka Walimu wakuu kuhakikisha kuwa kambi zinazoshughulikia wanafunzi lazima kuwepo walimu wasimamizi na kuhakikisha kambi zote zinakuwa na mazingira mazuri ya kuridhisha.
Amesema haitaruhusika kambi yeyote bila ya kuwepo mwalimu msimamizi ambapo pia amewataka kuacha kuwachanganya wanafunzi wa kike na wa kiume pamoja ili kuepusha vishawishi vitakavyoweza kuwaharibia masomo yao.
Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amewataka Walimu kutovunjika moyo kutokana na ugumu wa kazi na badala yake kuwa na uzalendo wa kujitolea ili kuleta maendeleo katika Elimu.
Amesema Wizara ya Elimu itaendelea kushirikiana na walimu pamoja na wazazi ili kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi unaongezeka na kuzitokomeza zero Zanzibar.
Akitolea ufafanuzi juu ya wanafunzi waliofeli kidatu cha pili na waliotakiwa kurejea darasa, Naibu Katibu Mkuu Taaluma Bi Madina Mjaka Mwinyi amesema ni lazima wanafunzi hao warudi Skuli kuendelea na masomo yao kwa kuwapangia utaratibu maalum na sio kubaki nyumbani, kwani ni haki yao kuendelea na masomo hadi kidatu cha nne.








Comments