Mjawiri ahimiza uwajibikaji.

VIONGOZI wametakiwa kutokuwa mfano wa watu wanaofanya vitendo vya uharibifu au  ukiukwaji wa  sheria katika maeneo yao ya kazi na jamii,badala yake wafuate maadili na taratibu za  uongozi.
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri, alitoa wito huo wakati akizungumza na viongozi na watendaji mbali mbali wa serikali katika ukumbi wa  Idrissa Abdulwakili, Kikwajuni.
Alisema kipimo cha kiongozi bora ni kuhakikisha uwajibika kazini pamoja na kuzingatia maadili,miongozo na taratibu.
Aidha alisema, ili kupatikane tija zaidi lazima viongozi na watendaji wajitambue na kujiheshimu katika utoaji wa huduma kwa wananchi kwani kufanya hivyo ni kufuata misingi ya utawala bora.
Alihimiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano,kubadilishana uzoefu na viongozi kujikubalisha kukosolewa na kupokea ushauri kutoka kwa watendaji wengine hasa ikizingatiwa watu wote wanajenga nyumba moja.
Mbali na hilo, alisema ugatuzi isiwe chanzo cha kuchangia migogoro na mivutano miongoni mwao badala yake wakubaliane kushirikiana na kutambua kwamba ni  kipindi hiki cha mpito kinahitaji zaidi ufanisi.
Alisema ugatuzi umedhamiria kuimarisha huduma bora kwa wananchi na sio kuwaonea watu hivyo ni wajibu wa kila mtendaji kutimiza dhamana aliyokabidhiwa kwa maslahi ya jamii na taifa kwa jumla.
Zanzibarleo.

Comments