
WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk. Sira Ubwa Mamboya amewataka wadau wa sekta ya usafiri barabarani kuandaa mikakati itakayohakikisha wanaotumia usafiri wa daladala wanaondokana na changamoto za usafiri huo.
Dk. Sira alieleza hayo jana alipokutana na wadau wa sekta ya usafiri barabarani wakiwemo Polisi, Tawala za Mikoa na Idara ya Usafiri na Leseni katika ukumbi wa wizara hiyo Kisauni wilaya ya Magharibi ‘B’.
Alisema nguvu za pamoja zinahitajika kwa sasa ili kuondoa utaratibu usioridhisha unaofanywa na baadhi ya waendesha daladala ambao umekua kero kwa abiria na wananchi kwa ujumla.
Waziri huyo alisema amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi hususani wanafunzi juu ya kero ya kushushwa njiani kabla ya kufika katika vituo vyao wanavyotakiwa kushuka na kutozwa nauli kubwa kinyume na sheria.
Alisema ametoa angalizo maalumu kwa madereva, ambapo kuanzia sasa dereva yeyote atakae ripotiwa kujihusisha na vitendo hivyo atachukuliwa hatua za kisheria na kamwe hakutakuwa na muhali dhidi yake.
Aidha alisema amekua akipokea malalamiko ya wazazi kwa watoto wao wamekua wakifika majumbani saa 4 usiku kutokana na shida ya usafiri huo na wakati mwengine kushushwa njiani jambo ambalo limekua likiwatia hofu wazazi hao.
Kwa upande wake Mkurugezi wa Idara ya Usafiri na Leseni, Suleiman Kirobo, alisema idara hiyo imekua ikilifuatilia kwa makini suala hilo na walichogundua ni tamaa ya fedha na uhaba wa gari za daladala katika baadhi ya njia.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa kuondolewa zamu kwa njia zenye upungufu wa gari ikiwemo njia ya Mwera Kianga, Fuoni, Chuo Kikuu, Kwarara, Mambo sasa na Nyarugusu kwa vile njia hizi ndizo zinazolalamikiwa kuwepo kwa vitendo vya aina hiyo.
Naye Z.T.O, Robart Hussein alikiri kuwepo kwa changamoto hizo jambo ambalo alisema kama jeshi la polisi wanalazimika wakati mwengine kutumia busara zaidi wakati wa usimamiaji wa sheria.
Aidha alisema licha ya kuwa jeshi lake kukabiliwa na changamoto ya vitendea kazi kama pikipiki na gari kwa ajili ya doria, lakini wanahakikisha kwenda sambamba na madereva hao ili kuhakikisha hakuna abiria ama mwananchi anapata kadhia yoyote.
Comments