
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) kina dhima ya kutoa taaluma bora inayoambatana na kufanya tafiti kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizomo katika jamii.
Dk. Shein ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) aliyasema hayo jana katika mahafali ya 14 ya Chuo Kikuu hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo ndani ya kampasi ya Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema kuwa kufanya tafiti mbali mbali ni miongoni mwa majukumu ya msingi ya vyuo vikuu jambo ambalo hutoa mchango wa chuo kitaaluma na kupandisha hadhi ya ubora wa chuo chenyewe.
Alikihimiza chuo hicho kuendelee kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania (COSTECH), ambayo ina wajibu wa kuwawezesha watafiti mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar kufanya tafiti wanazozikusudia.
Aliongeza kuwa chuo hicho kina wajibu wa kutafuta fedha za kufanya tafiti kutoka vyanzo mbali mbali kwani utafiti ni miongoni mwa majukumu ya chuo hicho hasa ikizingatiwa kuwa hakuna maendeleo bila ya utafiti.
Alieleza kuwa utafiti ni ngazi muhimu kwa Wanachuo wa mafunzo ya uzamili na uzamivu ambao huwasaidia kuhitimu masomo yao, na kukihimiza chuo hicho kujiandaa kuchapisha majarida ya kitaaluma ambayo wahadhiri na wanachuo wa ngazi ya uzamili na uzamivu watapata fursa ya kutuma makala zao zinazotokana na tafiti walizofanya.
Aidha, aliutaka uongozi wa chuo hicho kuwaweka sawa baadhi ya wahadhiri wachache ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo pamoja na wafanyakazi wote wanaojaribu kufanya kazi zao kinyume na utaratibu.
Alisema wahadhiri, walimu na wafanyakazi wa namna hiyo hawatimizi wajibu wao vizuri na hawachagii maendeleo ya chuo kwani wafanyakazi wa namna hiyo hawana uzalendo “Si wazalendo na hawastahiki wajigambe kuwa ni wahadhiri wa SUZA. SUZA ni chuo cha watu wenye kuyapenda maendeleo ya viongozi wa baadae”,alisisitiza.
Comments