
KATIBU Mkuu wizara ya Afya, Asha Ali Abdulla amesema Cuba imejijengea umaarufu mkubwa duniani kwa kuwa na wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali kwenye sekta ya afya.
Katibu huyo alieleza hayo alipooiongoza timu ya wakurugenzi wa wizara yake kwenye mazungumzo na uongozi wa taasisi ya kitaifa ya utafiti na matibabu ya maradhi ya saratani na mionzi ya nchini Cuba.
Mazungumzo hayo yalifanyika katika jengo la makao makuu ya taasisi hiyo yaliyopo mjini Havana nchini, Cuba wakiwa katika ziara ya siku nne ya kujifunza mbinu na masuala mbalimbali ya afya.
Katibu huyo alisema kutokana na hali hiyo, Zanzibar imekuwa moja ya nchi yenye kunufaika na kupata misaada mbalimbali kwenye sekta ya afya kutoka Cuba ikiwemo vijana wa Zanzibar kujifunza fani mbalimbali za afya nchini humo.
Asha alisema lengo la kuwapeleka vijana wa Zanzibar kwenda kupata mafunzo nchini Cuba ni kuongeza wataalamu wa ndani ambao watasaidia kuwapa wananchi huduma bora za afya.
Alisema Zanzibar imeanzisha kitengo cha matibabu ya saratani ambacho kitahitaji kupata msukumo wa kitaaluma kutoka kwa wataalamu waliobobea wa fani hiyo, akitolea mfano wataalamu wa taasisi kitaifa ya tiba ya saratani ya Cuba.
Katibu huyo alichukua fursa hiyo kuishuruku Cuba kupitia taasisi zake mbali mbali za kiafya kwa jitihada zake inazozichukua katika kiunga mkono Zanzibar kwenye sekta hiyo hasa utolewaji wa mafunzo ya juu kwa watumishi afya visiwani Zanzibar.
“Kitengo cha tiba ya maradhi ya saratani kwa Zanzibar bado kipya nadhani wataalamu wa Cuba wanaweza kusaidia mbinu na taaluma katika kuona mpango huo unafanikiwa kwa faida ya ustawi wa wananchi wote”, alisema Asha.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Mayasa aliushauri uongozi wa taasisi ya utafiti na matibabu ya maradhi ya saratani na mionzi ya Cuba kujenga ushirikiano na Zanzibar katika masuala ya utafiti, ufundishaji wa madaktari na wauguzi ambao wako katika Kktengo cha saratani.
Zanzibar.
Comments