Waziri wa Afya Zanzibar aagiza utafiti maradhi ya kinywa, meno.

WAZIRI wa Afya, Hamad Rashid Mohammed amewataka madaktari kufanya utafiti wa kina ili kujua kiwango cha maradhi ya kinywa na meno na namna ya kupunguza maradhi hayo.
Waziri Hamad aliyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno duniani iliyofanyika Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge mjini Zanzibar.
Alisema utafiti huo utaweza kusaidia kutoa taaluma zaidi kwa walimu wanaofundisha watoto wakiwa skuli na hivyo kuwajengea uwezo wa kujikinga na matatizo ya kutoboka kwa meno na kuvimba ufizi.
Alifahamisha kuwa kufanyika kwa utafiti huo kutasaidia kupatikana kwa takwimu sahihi na kuweza kujua ukubwa wa maradhi hayo, hali ambayo itasaidia kupatikana kwa ufumbuzi.
Aidha aliwataka wananchi kuvitumia vituo vya afya na hospitali za serikali kupata huduma bora ili kuondoa matatizo yanayowakabili.
“Nia ya serikali ni kuwa na taifa la watu wenye afya ni vyema kupima afya zetu angalau mara mbili kwa mwaka katika vituo vya afya vilivyokaribu nasi”, alieleza waazri Hamad.
Aidha aliwaomba wananchi kufanya usafi wa kinywa pamoja na kuwafundisha watoto namna ya kupiga msuwaki ili kuepuka matatizo kutoboka kwa meno na kutoa harufu katika kinywa.
“Asilimia 90 ya matibabu ya maradhi haya tunayo wenyewe, tiba zaidi ni kuwa wasafi, hivyo nawaomba sana kuzingatia usafi maana afya ni usafi”, alisisitiza waziri.
Alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi kuchangia damu kwa lengo la kusaidia jamii na kuokoa maisha ya wagonjwa ambao wanakabiliwa na tatizo la kupoteza damu.
Aidha aliwasisitiza madaktari na wahudumu wa afya kuwa wazalendo na kufanyakazi kwa bidii pamoja na lugha nzuri wakati wa kuwahudumia wananchi.
Nae mkuu wa kitengo cha meno na kinywa katika hospitali ya Mnazimmoja, Dk. Semeni Shaaban Mohamed alisema asilimia 90 ya wananchi wana matatizo ya meno ni vyema kwa jamii kuwa na utamaduni wa chunguza afya ya meno ili kuepuka madhara ya kutoboka na kung’oka.
Zanzibarleo.

Comments