Waziri, balozi wajadili kuimarisha utalii.

AFRIKA Kusini na Zanzibar zina nafasi kubwa ya kuimarisha ushirikiano katika kuitumia sekta ya utalii kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi hizo.
Akizungumza na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania Thami Mseleku aliyemtembelea ofisini kwake jana waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, alisema hilo litawezekana kwa kuanzisha jukwaa la pamoja litakalojikita katika kuinua sekta hiyo.
Alitaka jukwaa hilo lijumuishe wizara mbalimbali za serikali na taasisi binafsi zinazojishughulisha na utalii, kama vile Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar, Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) na nyengine.
Alieleza kuwa, kwa kuwepo jukwaa hilo ambayo ni fikra ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, nchi hizo zitaweza kubadilishana uzoefu, kujadiliana kwa kina na kupendekeza njia bora zaidi za kuinua utalii ili uwe na tija zaidi kwa pande zote mbili.
Alimshauri balozi huyo kuangalia uwezekano wa kulitaka Shirika la Ndege la Afrika Kusini (Mango), kuongeza idadi ya safari zake za moja kwa moja Zanzibar ili kuleta wageni wengi zaidi na hivyo kutunisha mfuko wa fedha za kigeni.
Aidha alimtaka kuwashawishi wawekezaji zaidi kutoka Afrika Kusini kuja kuwekeza miradi yao ya sekta mbalimbali hususan utalii, akikitaja kisiwa cha Pemba mbali na maeneo mengine ya Zanzibar, kuwa kimejaa vivutio vya maumbile na vya kipekee vinavyoweza kuwapendeza watalii watakaofika.

Comments