Wazazi wawarejesha vijana wao Somalia ili wasichomwe visu Uingereza.

Wazazi wawarejesha vijana wao Somalia ili wasichomwe visu Uingereza
Kutokana na kushtadi hujuma za visu nchini Uingereza, wazazi wa Kisomali wamewarejesha kwa wingi vijana wao nchini Somalia.

Wawakilishi wa jamii ya Wasomali kaskazini mwa London wamenukuliwa na gazeti la The Observer wakisema kuwa, mamia ya vijana wa Kisomali ima wamerejeshwa na wazazi wao nchini Somalia au Kenya wakihofiwa kuwa watauawa au kushambuliwa kwa visu nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa Rakhia Ismail, Naibu Meya wa eneo la Islington mjini katikati mwa London amesema, "Kuwarejesha nyumbani ndilo chaguo la pekee la kuwanusuru." 
Alkhamisi iliyopita, kijana wa Kisomali kwa jina Ayub Hassan, aliyekuwa na umri wa miaka 17, aliuawa kwa kuchomwa kisu na kijana mzungu wa miaka 15, magharibi mwa London.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, mama wa Kisomali anayeishi kaskazini mwa London Ijumaa iliyopita alisafiri mjini Mombasa nchini Kenya kwa lengo la kumshawishi kijana wake wa miaka 19 asirejee nchini Uingereza, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na magenge ya wahalifu.
Kwa mujibu wa duru za kiusalama, watu 19 wameuawa kwa kuchomwa visu mjini London pekee tokea mwanzoni mwaka huu hadi sasa.

Comments