
WIZARA Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, itawazawadia zawadi ya fedha taslim walimu watakaoandika makala yenye kuhusiana na masuala ya utawala bora.
Waziri wa wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman aliyasema hayo wakati akizungumza na walimu wa msingi wanaofundisha somo la uraia huku Mazizini.
Alisema lengo la wizara ni kuhakikisha suala la utawala bora kwa viongozi, watendaji na wananchi linaendelea kutiliwa mkazo ili kuleta mafanikio zaidi katika utoaji wa huduma mbali mbali ikiwemo za kijamii, miundombinu na miradi mengine ya kimaendeleo.
Aidha alisema ni vyema kwa walimu hao kuhakikisha wanafatilia kwa karibu mambo mambo yaliyomo ndani ya jamii zilizowazunguka kwa kueleza jinsi gani maeneo hayo yanatekeleza utawala bora na changamoto zilizopo pamoja na mambo ambayo yanahitaji kuongezwa uwelewa kwa wananchi.
“Walimu nakuombeni fanyeni juhudi za kuandika makala za utawala bora mbali na zawadi mtakazozawadia pia itakujengeeni uwezo mkubwa wa kutambua utawala bora”, alisema.
Waziri huyo, alisema utekelezaji wa hilo utawezesha kuendelea kufanya tathmini endelevu sambamba na kuongeza wigo na kuwajenga wananchi wasimamie misingi ya utawala bora kuanzia ngazi ya familia hadi maeneo ya kazi.
Alisema kuimarika kwa utawala bora nchini utasaidia kupunguza vitendo vya udhalilishaji, rushwa na vyengine ambavyo vinachangia kuwanyima fursa na hali za msingi watu wanohitaji huduma.
Zanzibarleo.
Comments