
MKURUGENZI wa Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, Soud Mohammed amesema uwepo wa shughuli nyingi za binaadamu karibu na misitu unachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira ya misitu.
Alieleza hayo wakati akifungua kongamano lililowashirikisha wadau wa misitu na kamati za shehia lililofanyika kituo cha vitalu Mwanyanya, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya misitu duniani ambayo hufanyika kila ifikapo Machi 21 ya kila mwaka.
Alisema kuna tishio la uharibifu unaosababisha kupotea kwa misitu ya asili kutokana na ukataji ovyo na holela wa miti hiyo jambo ambalo linasabisha athari kubwa.
Alisema sensa ya miti iliofanywa mwaka 2013, imeonesha kuwa Zanzibar imepoteza karibu nusu ya minazi kwa kisingizio ya kilimo, makaazi na upasuaji mbao.
“Tunakata kuni na ukataji miti na kupelekea kukosa hewa na kama hatujakumbushana, tunaweza kukabiliwa na hali ya hatari”, alisema.
Alifahamisha kuwa Zanzibar misitu inayokaribia hekta 1,000 inapotea kila mwaka hali ambayo ni tishio kubwa hasa ikizingatiwa kuwa udogo wa ardhi ya Zanzibar.
Alisema serikali imekuwa inahifahi misitu kwa faida ya vizazi vilivyopo na baadae, hivyo ni vyema kila mmoja akatekeleza wajibu wake katika kulinda na kuheshimu misitu.
Nae ofisa misitu Rahika Mohammed Suleiman, alisema madhimisho ya siku misitu yana umuhimu mkubwa kwani inapatikana fursa ya kuelimishana juu ya athari za uharibifu wa misitu.
Alisema bila ya kuwepo mikakati ya kuitunzana kuilinda miti baada ya miaka miaka michache hali inaweza kuwa mbaya kutokana na kasi ya uharibifu wa misitu.
Nao wadau wa kongamano hilo walisema waliiomba idara kuweka mahakama ya misitu, ili kuweza kurahisisha kesi za watuhumiwa wa uharibifu wa rasilimali hiyo.
Zanzibarleo.
Comments