Samia aanika Dk. Shein alivyotekeleza ilani.

MAKAMU wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuna kila sababu ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kwani ametekeleza kwa umahiri mkubwa ilani ya uchaguzi na kuleta mafanikio makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kauli hiyo, aliitoa jana wakati akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na UWT, la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, kwa kutimiza miaka mitatu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, lilofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Verde Mtoni.
Alisema Dk. Shein amefanya kazi kubwa kusimamia ilani ya uchaguzi katika awamu yake ya pili iliyoanza mwaka 2015 hadi 2018 na kabla ya hapo alifanyakazi nzuri kuanzia mwaka 2010.
Alisema, kongamano sio tu la kumpongeza Dk. Shein katika uongozi wake bali pia ni kongamano la kutoa ushuhuda kwa yale mazuri yote yaliyofanyika ndani ya Zanzibar chini ya serikali ya CCM.
Aidha, alisema wananchi wa Zanzibar ni mashuhuda kwa kazi nzuri iliyofanyika nchini katika kipindi cha uongozi wa Dk. Shein, kwani Zanzibar imekuwa na maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu.
Alisema moja ya utekelezaji wa Dk. Shein katika uimarishaji wa huduma za afya, ambapo ameendeleza na kuimarisha kwa ufanisi mkubwa uamuzi uliotolewa Machi 3 mwaka 1965 wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume wa kuwapa wananchi wa Zanzibar matibabu bure.
Alibainisha kuwa, mfano wa hayo ni kuogezeka kwa bajeti ya wizara ya Afya mwaka 2018/2019, ambapo bajeti ya dawa ni bilioni 12.7 sambamba na kutoa pencheni kwa wazee waliotimia umri wa miaka 70.
Samia, alisema katika kukuza sekta ya afya, Dk. Shein ameshaanza ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa katika eneo la Binguni huku katika sekta ya elimu kuongezeka kwa skuli za maandalizi, msingi na sekondari.
Eneo jengine, alisema ni kuongezeka kwa vyuo vikuu, huku katika upande wa ujenzi na miundombinu serikali za CCM zimeweza kutengeneza barabara ambapo Dk. Shein ameendeleza juhudi hizo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Jendele – Cheju hadi Kaebona, Mgagadu- Kiwani na Likoni.

Comments