
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud amempongeza Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuteua watendaji wawili kutoka katika ofisi ya Mkoa huo jambo linaloonyesha kukubalika kwa utendaji wa watumishi wa ofisi yake.
Akizungumza kwenye hafla ya kuwashukuru na kuwapongeza waliokuwa Makatibu Tawala wa Mkoa huo iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uandishi wa Habari uliopo Kilimani mjini Zanzibar, Ayoub alisema uteuzi huo unatokana na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kuliko mshawishi Rais kuwapa majukumu mapya.
Alisema kuwa Katibu Tawala kunatoa nafasi ya kukutana na kutambua changamoto za wananchi moja kwa moja, hivyo bila ya uthubutu, busara na hekima katika utumishi, sio rahisi kupata uteuzi katika nafasi za juu.
“Unapopata uteuzi maana yake aliyekuteua amekuamini, hivyo nawaomba mkatekeleze majukumu yenu kwa juhudi na maarifa ili kulipa imani aliyowapa Mheshimiwa Rais kwani imani hulipwa imani na sio vyenginevyo”, alisema Mkuu huyo.
Aidha aliwapongeza na kuwashukuru wateule hao Ali Juma Silima aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi katika wizara ya Katiba na Sharia na Hamida Mussa Khamis aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Kati, ambapo aliahidi kuwapa ushirikiano kila watakapohitaji.
Aidha Ayuob alitoa rai kwa watumishi wengine kufanyakazi kwa kuzingatia taratibu za utumishi na msingi wa huduma zinazowastahikia badala ya kuzingatia maslahi binafsi.
“Wapo baadhi ya viongozi na watendaji wanaochagua watu au viongozi wa kuwaheshimu na kuwahudumia bila kuzingatia misingi ya kazi na majukumu yao kwani kila mmoja ana mchango katika kufanikisha wajibu wa mwengine”, alisema Ayoub.
Akisoma risala kwa niaba ya wafanyakazi wenzake Ofisa habari wa Mkoa huo Mohammed Ali Juma, alisema uteuzi wa watendaji hao umeongezea sifa Mkoa na kuthibitisha kuwa mkoa huo una watendaji wenye sifa na uwezo wa kulitumikia taifa.
Comments