Ndugai kulibeba suala la sukari ya Mahonda.

SPIKA wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ameahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la soko la sukari ya Zanzibar na kuona inaingia katika soko la Tanzania bara.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na uongozi wa kiwanda cha Sukari Mahonda, wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, alipofika kwa ajili ya kuangalia maendelea ya kiwanda hicho.
Alisema atahakikisha suala hilo analifikisha katika kamati za kitaalam za bunge ili kuona changamoto hiyo inaondoka na kuona sukari hiyo inaingia katika soko la Tanzania bara.
Spika Ndugai, alisema suala la kiwanda hicho limekuwa likizungumzwa sana katika vikao vya bunge na wabunge wanaotoka Zanzibar, hivyo linawezekana kupatiwa ufumbuzi na bunge kuweza kuidhinisha kutokana na nchi kuwa na lengo moja la kukuza mapato kupitia uchumi wa viwanda.
Alisema upo uwezekano mkubwa wa bidhaa hiyo kuona inauzwa Zanzibar na Tanzania bara bila usumbufu ili kusaidia kiwanda hicho kupata fedha kwa ajili ya kujiendesha.
Aidha aliwapongeza wamiliki wa kiwanda hicho kuitikia wito wa serikali kuendeleza viwanda kwa lengo la kukuza ajira za vijana na kuleta mabadiliko ya kiuchumi nchini
Meneja miradi wa kiwanda hicho, Frank Hubert Mtu alisema, kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto ya soko la bidhaa hiyo kutokana na kiwanda hicho kuzalisha kwa gharama zaidi ya viwanda vilivyokuwepo Tanzania bara, ikiwemo gharama za kiuendeshaji.
Akizungumzia changamoto nyengine meneja huyo, alisema hakuna sheria ya ushuru wa forodha, sheria ya kodi au sheria ya sukari inayozuia sukari inayozalishwa Zanzibar kuingia bara.
“Sisi watanzania tulioamua kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano katika azima yake ya kuifanya serikali ya viwanda ifikiwe basi tunaomba tuweze kufurahia uhuru wa masoko ya bidhaa yetu bila ya kuvunja sheria na taratibu za nchi”, alisema.
Zanzibarleo.

Comments