
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amewasili kisiwani Unguja, Zanzibar jana jioni Jumatano Machi 20, 2019 akitokea Dar es Salaam.
Kuwasili kwa Maalim Seif visiwani kumewafanya watu wengi kutaka kumsikia kwa mara ya kwanza atazungumza nini au atafanya shughuli gani ya kisiasa baada ya kuwa amejiunga na chama kipya cha ACT- Wazalendo.
Juzi Jumatatu, Maalim Seif pamoja na viongozi wengine wa CUF walikabidhiwa kadi za uanachama za ACT- Wazalendo katika shughuli iliyofanyikia makao makuu ya ACT- Wazalendo, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Mwanasiasa huyo aliyesafiri kwa boti, katika bandari ya Malindi mjini Unguja amepokelewa na aliyekuwa Naibu katubu mkuu CUF- Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui na baadhi ya wananchi na wanachama wapya wa ACT- Wazalendo.
Katika bandari hiyo, Maalim Seif hakuzungumza lolote licha ya uwepo wa baadhi ya waandishi wa habari waliokuwapo.
Uamuzi wa Maalim Seif kutangaza kuhamia ACT- Wazalendo aliuchukua Jumatatu iliyopita ya Machi 18, 2019 ikiwa ni muda mchache kupita tangu Mahakama Kuu ya Tanzania kumhalalisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF.
Mwananchi.
Comments