
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Kizimbani, imesema ipo katika hatua za awali kutafuta mbegu za mpunga zinazohimili katika mabonde yanayoingia maji chumvi nchini.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Suleiman Shehe Mohammed, alisema hayo ofisini kwake Kizimbani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali walipofanya ziara ya kutembelea miradi ya utafiti wa kilimo iliyofadhiliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Alisema wameamua kufanya utafiti huo kutoakana na maeneo mengi hivi sasa ya visiwa vya Zanzibar yamezungukwa na maji chumvi, hivyo kunauwezekano mkubwa wa kusababisha kukosekana kwa maeneo ya kilimo.
Mkurugenzi huyo alifahamisha kwamba, kufanywa kwa utafiti huo kutasaidia kubaini mbegu ambayo itaweza kuhimili katika maeneo hayo na kuweza kupatikana chakula ambacho kitakuwa na tija kwa jamii.
Alibainisha kwamba, utafiti huo utajumuisha kutafuta mbegu bora ambayo itahimili maji chumvi na maradhi ili kuisaidia jamii kuyatumia maeneo hayo kwa urahisi na kuondosha hofu.
“Utafiti huo utajumuisha kutafuta mbegu ambayo itamudu mahitaji ya maji chumvi ili kuwasaidia wananchi kupata maeneo ya kilimo kwa sababu maeneo mengi hivi sasa yanaingia maji hayo”, alisema.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo, alibainisha kwamba utafiti huo upo katika hatua ya awali, hivyo ni mategemeo yao kwamba kukamilika kwake kutasaidia kuondosha uhaba wa maeneo ya kilimo nchini na kukidhi mahitaji ya chakula.
Ziara hiyo ya siku moja iliyowashirikisha waandishi wa habari imeandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH, ikiwa na lengo la kukagua miradi ya kilimo iliyofadhiliwa na tume hiyo.
Zanzibarleo.
Comments