
KATIBU Mkuu wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe amesema nguvu za pamoja zinahitaji kati ya wizara yake, mjezi wa barabara ya Bububu – Mkokotoni na mshauri elekezi ili kuhakikisha mradi huo unamalizika kwa wakati na kwa kiwango.
Mustafa alieleza hayo jana alipokutana na timu hizo mbili kwa lengo la kupitia ripoti ya utekelezaji wa mradi huo, huko katika ukumbi wa mikutano wizarani Kisauni.
Aidha alisema lengo la kukutana na wahusika hao ni kuangalia mradi umefikia wapi na changamoto zinazoukabili mradi huo na kutafuta njia za kutatua ili mradi huo uendelee kama ulivyokusudiwa.
Hata hivyo, alimtaka mkandarasi na mshauri elekezi kuwa kitu kimoja katika kuhakikisha mradi huo unakwenda sambamba na malengo na matakwa ya serikali na sio kuwa na tofauti kati yao.
Alisema mradi huo ndio una fadhiliwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia, hata hivyo serikali mwisho wa siku wanatakiwa kulipa deni hilo ambapo alifahamisha kuwa fedha hizo zitakazolipwa zinatokana na kodi za wazanzibari, kwa hiyo lazima wawe makini katika ujenzi wa mradi huo.
Mustafa aliwaeleza kuwa Zanzibar inaelekea katika msimu wa mvua za masika hivyo alishauri sehemu ambazo hazina matatizo ya kiufundi wazikamilishe kabla mvua hizo hazijanza.
Alisema wakati umefika kwa pande zote tatu kusaidiana kimaarifa, kiufundi na kinadharia ili kuona mradi huo hautokua kikwazo kwa wananchi na wanasiasa pamoja na serikali kwa ujumla.
Kwa upande wake meneja wa mradi huo, Zhang Oijum alisema ratiba ya ujenzi ipo nyuma kutoka na sababu mbalimbali, lakini watahakikisha mradi huo unakwenda vizuri na kumaliza kwa wakati.
Kwa upande wake mshauri elekezi kutoka kampuni ya Gauff, Yussuf S. Yussuf aliiomba wizara kusafisha maeneo mengine ya mradi huo ambayo yanatarajiwa kujengwa barabara ikiwemo eneo la Pale – Kiongele, Muyuni Matwemwe na Fuoni Kombeni ili waweze kumkabidhi mkandarasi aendelee na kazi.
Zanzibar.
Comments