
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameitaka Kamisheni ya Utalii kutoa elimu ya historia ya utalii hapa visiwani, ili kujua unakotoka, unakokwenda na hatua zilizofikiwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo, alipokutana na uongozi wa wizara ya Habari, Utalii, na Mambo ya Kale uliofuatana na uongozi wa Kamisheni ya Utalii na Makamishna wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, katika kikao kilichofanyika ikulu mjini Zanzibar.
Alieleza kujulikana kwa historia ya utalii hapa Zanzibar kutasaidia kufahamika lengo lililokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuelewa jinsi utalii ulivyokuwa hapo siku za nyuma, jinsi ulivyo hivi sasa na mafanikio yaliyofikiwa.
Alisema sekta ya utalii imekuja baada ya zao la karafuu kushuka thamani na ndipo marehemu mzee Aboud Jumbe Mwinyi akaona haja ya kuiimarisha sekta hiyo na baadhi ya mazao mengine ya viungo.
Alieleza kuwa tokea kipindi hicho sekta ya utalii imeweza kuimarika kwa kiasi kikubwa kwa kuwepo vivutio kadhaa hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar inajitangaza yenyewe kutokana na vivutio vilivyopo.
Aliongeza kuwa hivi sasa Zanzibar iko vizuri kiutalii ikilinganishwa ilivyokuwa hapo siku za nyuma, kwani utalii wa Zanzibar unasifika zaidi duniani kote na kuwapelekea watalii kuitembelea Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa hivi sasa utalii wa Zanzibar unaongozwa na sheria ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2012 kwa lengo la kuufanya utalii uwe kwa wote kwani ndio uchumi wa Zanzibar.
Alieleza kuwa sheria ndio ngao kubwa ya kuendesha Kamisheni ya Utalii, hivyo alisisitiza Kamisheni kuzingatia na kuifanyia kazi sheria hiyo na kanuni zake ili iweze kuwasaidia kuendeleza sekta hiyo.
Alisema maamuzi ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa sekta zote zinabebwa na sekta ya utalii pamoja na kuonyesha umakini wake katika sekta hiyo na kuipa dhamana Kamisheni hiyo.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mashirikiano kati ya waziri, wizara, bodi, kamisheni na makamishna kwa lengo la kuiimarisha sekta ya utalii ambayo ndio ukombozi wa uchumi wa Zanzibar.
Comments