Dk. Shein: Migogoro ya ardhi imefikia pabaya.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema licha ya kuwepo sheria tisa zinazohusiana na matumizi bora ya ardhi hapa Zanzibar, lakini wapo watu hawazifuati sheria hizo.
Dk. Shein aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa semina ya siku moja kuhusu masuala ya ardhi na rasilimali zisizorejesheka, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni mjini Zanzibar.
Alisema lengo la serikali kuhakikisha ardhi inatumika hapa Zanzibar kwa nyakati mbali mbali, limesababisha kuwa na tisa kuhusiana na matumizi bora na endelevu ya rasilimali hiyo na kuwepo kwa rasilimali zisizorejesheka kama vile mchanga, mawe, udongo na misitu, hata hivyo sheria hizo hazifuatwi.
Alizitaja baadhi ya sheria hizo ni sheria ya Matumizi ya Ardhi Namba 12 ya mwaka 1992, sheria ya Uhaulishaji wa Ardhi Namba 8 ya mwaka 1994 na sheria ya Mahakama ya Ardhi Namba 7 ya mwaka 1994 ambayo ndiyo inayohusiana na uanzishwaji wa Mahakama ya Ardhi.
Alisema katika ziara aliyoifanya katika wilaya za Unguja na Pemba mwezi uliopita ameweza kufahamu mengi kuhusiana na kadhia ya kuvunjwa kwa sheria zinazohusiana na ardhi.
Dk. Shein alisema kwa bahati mbaya wavunjaji wa sheria hizo hufanywa na viongozi na watendaji wa serikali pamoja na wananchi wa kawaida.
“Taarifa za wilaya zilizowasilishwa kwangu zote zimethibitisha kuendelea kuibuka kwa migogoro mipya ya ardhi katika wilaya ambazo inatofautiana kwa idadi na kwa aina yake baina ya wilaya na wilaya…
…Nna taarifa kwamba ipo migogoro ya uvamizi wa maeneo ya serikali, ipo migogoro baina ya wananchi na wawekezaji na mingine kadhaa”, alisema Dk. Shein.
Alibainisha kuwa jambo jengine ni kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo yanayochimbwa mchanga aliyoyatembelea, sambamba na kuwepo kwa upungufu wa mchanga.
Alieleza kuwa katika maeneo la Donge Chechele, Pangatupu na Kiombamvua kwa Unguja na Finya (Selem) na Shumba Viamboni kwa uapnde wa Pemba, amejionea hali halisi ya rasilimali hiyo ya mchanga na kusisitiza kuwa mchanga ni mali ya serikali, hivyo ni mali ya wananchi wote.

Comments