
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza azma ya Umoja wa Mataifa (UN) kupitia programu ya kujitolea ya Umoja huo (UNV) kwa kuendea kuiunga mkono Zanzibar katika shughuli za maendeleo.
Dk. Shein alieleza hayo jana ikulu mjini Zanzibar alipofanya mazungumzo na mratibu mkuu wa programu ya kujitolea ya Umoja wa Mataifa (UNV) Oliver Adam, aliyefika Zanzibar kwa lengo la kuimarisha mashirikiano baina ya pande mbili hizo.
Alimueleza Mratibu huyo kuwa (UNV) ni programu muhimu iliyo chini ya Umoja wa Mataifa ambayo ina umuhimu mkubwa katika kuendeleza shughuli mbali mbali za maendeleo hapa Zanzibar.
Alisema progmu hiyo imeanza miaka mingi na kuweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza na kuunga mkono juhudi za serikali katika shughuli za maendeleo ikiwemo sekta ya afya na kilimo.
Aidha, alimueleza mkuu huyo kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha kituo cha ujasiriamali ambacho kinatoa mafunzo kwa vijana ya kazi za aina mbali mbali ambapo kuna haja ya kukiongezea uwezo na kuwapatia mtaji vijana hao ili wanaufaike na elimu wanayoipata.
Alisisitiza kuwa kuna haja ya kuweka mikakati maalum ya kuwajengea uwezo vijana wote wa Unguja na Pemba, ili waweze kujiajiri wenyewe kwa kuwapa mikopo itakayowasaidia kujiendeleza.
Dk. Shein alisisitiza haja ya programu hiyo kuunga mkono katika kuongeza nguvu kwa kupata walimu wa masomo ya sayansi kwa skuli za sekondari za Zanzibar ambao bado wanahitajika.
Alieleza kuwa licha ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka mikakati maalum na kuyapa kipaumbele masomo ya sayansi kwa kuwashajiisha wanafunzi kuyasoma kwa bidii na hatimae kujiendeleza katika vyuo vyake vitatu vikuu vilivyopo hapa nchini.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza uhaba wa madaktari wa upasuaji ambao bado wanahitajika katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini licha ya juhudi zinazochukuliwa na serikali za kuwasomesha wataalamu wa kada hiyo.
Comments