Baraza kuu CUF lamng’oa Maalim Seif.

HATIMAYE baraza kuu la Uongozi la chama cha CUF Tanzania, chini ya Mwenyekiti wake Prof. Ibrahim Lipumba limempitisha, kukubali na kuliidhinisha jina la Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu mpya wa chama hicho.
Katibu mkuu huyo anachukua nafasi ya mwanasiasa wa muda mrefu aliyeshika madaraka mbalimbali hapa nchini, Maalim Seif Hamad ambaye hakugombea nafasi yake kutokana na mgogoro mkubwa ulipo baina yake na kambi ya mwenyekiti Prof. Lipumba.
Mwenyekiti huyo wa CUF, alimtangaza Khalifa ambaye ni mbunge wa zamani wa jimbo la Gando, katika mkutano wa baraza kuu la chama hicho uliofanyika jana makao makuu ya chama hicho yaliyopo, Buguruni jijini Dar es Salaam.
Mbali na Khalifa, Prof. Lipumba pia alimtangaza mbunge wa jimbo la Kaliua mkoani Tabora, Magdalena Sakaya kuwa naibu katibu mkuu Bara, ambapo Fakhi Suleiman Khatib anakuwa naibu katibu mkuu Zanzibar.
Kabla ya jina la Khalifa kuchomoza, Prof. Lipumba aliwasilisha majina matatu ya nafasi ya katibu mkuu na matatu ya nafasi ya manaibu katibu wakuu Bara na Zanzibar kwa ajili ya kujadiliwa kabla ya kupendekezwa moja kushika nafasi hiyo.
Katibu mkuu huyo mpya ambaye atakuwa mrithi wa Maalim Seif, alipatikana baada ya kuchaguliwa na baraza kuu la uongozi la CUF lililokutana juzi jijini Dar es Salaam.
Itakumbukwa kuwa baraza hilo kuu la uongozi la CUF lililokutana juzi kwa ajili ya kujadili jina la katibu mkuu mpya, ambapo ilionekana dhahiri ndio mwisho wa ‘ufalme’ wa Maalim Seif ndani ya CUF ambaye kwa sasa anatofautiana kwa kiasi kikubwa na na mwenyekiti wake.
Aidha siku ya kwanza ya kikao cha baraza kuu la uongozi, kilipitisha mabadiliko ya katiba yanayoondoa katibu mkuu wa kuchaguliwa na kufanya nafasi hiyo iwe ya kuteuliwa, huku mwenyekiti akipewa mamlaka ya kuteua akishirikiana na makamu mwenyekiti wa bara na Zanzibar.
Hata hivyo, hatima ya viongozi hao wapya wa CUF akiwamo mwenyekiti Prof. Lipumba aliyechaguliwa na Jumatano iliyopita, itajulikana baada ya hukumu itakayotolewa kesho na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Comments