
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo juhudi zinazohitajika kuchukuliwa kwa nchi za Afrika, ili kukabiliana na changamoto zinazolikabili bara hilo.
Balozi Seif alieleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na mabalozi wa mataifa ya bara la Afrika wanaoziwakilisha nchi zao nchini Cuba, walipofika kumsalimia na kubadilishana mawazo katika ukumbi wa hoteli National iliyopo mjini Havana nchini Cuba.
Alisema mataifa ya Afrika muda wote lazima yaendelee kushirikiana kidugu kutokana na historia yao inayofanana ya kiutamaduni, kisiasa, mila na hata kiuchumi na kwamba hata changamoto zinazozikumba nchi hizo zinafanana.
Makamu huyo alisema wakati umefika kwa Waafrika kubadilika na kujitegemea wenye ili kuepuka mfumo wa utegemezi unaosababisha baadhi ya wafadhili wa kigeni kulazimisha kufanywa mambo yanayokwenda kinyume na mila na silka za mataifa hayo.
Alisema njia nzuri ya mashirikiano kwa mataifa ya Afrika ni kutumia fursa za jumuiya za kikanda za ushirikiano ambazo zitakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo.
Aliwaeleza mabalozi hao wa Afrika walioko Cuba kushikamana katika kuliona bara lao linafunguka kiuchumi kwa kuzishawishi kampuni na taasisi za uwekezaji kuelekeza miradi yao barani humo.
Balozi Seif, alieleza kwamba bara la Afrika litaendelea kuwa na matumaini makubwa kutokana na rasilmali zake zinazopaswa kutangazwa na mabalozi hao katika kazi zao wakizingatia pia mfumo wa kuwa na jumuiya zao za ofisi za kibalozi ndani ya majukumu yao ya kidiplomasia.
“Nakumbuka nikiwa mwanadiplomasia nchini Misri tuliwahi kuwa na taasisi yetu ya ushirikiano wa mabalozi tuliofanya kazi nchini Misri tukiita Afro Asian Diplomatic Union ambayo ilisaidia kutuunganisha wanadiplomasia”, alisema Balozi Seif.
Zanzibarleo.
Comments