
WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali, amewataka wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kushirikiana kupiga vita rushwa nchini ili kuepusha jamii na madhara ya kiuchumi.
Alisema kujenga jamii inayoheshimu sheria na kujiepusha na rushwa kutapunguza uzalishaji na uingizaji wa bidhaa zilizo chini ya viwango ili kumlinda mtumiaji.
Balozi Amina aliyasema hayo wakati akifungua warsha ya kuadhimisha siku ya viwango Afrika iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni iliyoambatana na utoaji wa zawadi kwa washindi wa shindano la insha lililohusisha taasisi za elimu ya juu.
Alisema siku hiyo inayoadhimishwa kila ifikapo Machi 21 kila mwaka imelenga kujenga uelewa wa jamii katika maswala ya viwango na kuimarisha mifumo ya utekelezaji na utendaji ya taasisi za viwango barani Afrika.
Alisema rushwa imezorotesha maendeleo jamii nyingi ulimwenguni na kupelekea madhara kwa wananchi kutokana na kukosa huduma bora na kuadimika kwa soko hasa kwa bidhaa zinazioalishwa au kuingizwa nchini bila ya kuwa na viwango.
“Vitendo vya rushwa katika jamii zetu vinatendeka katika nyanja mbali mbali hivyo ipo haja ya kila ngazi katika uendeshaji wa uchumi kuzingatia umuhimu wa kujiepusha na rushwa”, alieleza Balozi Amina.
Aidha alipongeza hatua ya shirikisho la taasisi za viwango barani Afrika (ARSO) na taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) kwa kuamua kutanua wigo wa elimu ya viwango katika taasisi za elimu ya juu.
“Ninaamini wanafunzi wamejifunza juu ya umuhimu wa viwango na namna ya kuunganisha mapambano ya rushwa hapa Zanzibar na ninafurahi sana kuona ZBS (taasisi ya viwango Zanzibar) imepeleka somo la viwango kwa vijana wa taasisi za elimu kwa sababu huko ndipo watapotoka viongozi, wanasayansi na wachumi”, alisema Balozi Amina.
Awali akitoa maelezo kuhusu maadhimisho hayo, Mkurugegenzi Mkuu wa ZBS Khatib Mwadin Khatib, alisema katika maadhimisho hayo shirika la viwango Afrika limechagua ujumbe maalum unaounganisha shughuli za udhibiti wa viwango na mapambano dhidi ya rushwa.
Zanzibarleo.
Comments