Alipa faini kujinusuru kifungo kwa kuchimba mchanga.

SAID Ali Hassan (45), mkaazi wa Matarumbeta, ametozwa faini ya shilingi 1,100,000 katika Mahakama ya Mwanzo Malindi, baada ya kukubali kosa aliloshtakiwa mahakamani hapo.
Mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na kosa la uharibifu wa mazingira kwa kuchimba mchanga, alifikishwa mbele ya Hakimu Maisara Abdallah Maisara na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo, Suleiman Khalfan Masoud.
Ilidaiwa kuwa, Machi 9 mwaka huu majira ya saa 1:00 usiku, maeneo ya Kinazini  wilaya ya Mjini  Mkoa wa Mjini Magharib, alipatikana akichimba mchanga bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka husika, ambapo kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa kosa hilo ni kinyume na vifungu vya 24 (1) (2) (3), 25 (1) (2) (3) na 26 (1) (2) (3) ya mwaka 2017 sheria ya mazingira.
Baada ya kusomewa shitaka lake, mshitakiwa huyo, alilikubali bila ya kuacha shaka yoyote, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshtakiwa huyo.
Hata hivyo Mwendesha Mashitaka aliiomba mahakama impe adhabu kulingana na kosa alilopatikana nalo.
Hakimu Maisara mara baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili alimpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi milioni 1,100,000 au atumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.
Mshtakiwa huyo alilazimika kulipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda wa miezi sita.
Zanzibarleo.

Comments