Wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto imewashukuru waganga wa tiba asili na tiba mbadala kwa ushirikiano katika afya za binaadamu na maendeleo ya jamii kwa ujumla huku serikali ikiendelea kutambua umuhimu wa fani hiyo muhimu na kuwataka waganga wa tiba asili kuendelea kutoa ushirikianao katika zoezi la uhakiki ili waweze kufanya kazi kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na wizara ya afya.
Akizungumza na waganga wa tiba asili na tiba mbadala katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Njombe kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara hiyo, Mwenyekiti wa Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Bi. Hanifa Selengu iliyofika mkoani Njombe kwa lengo la kuunganisha nguvu na Serikali ya Mkoa katika kupata namna bora ya kukomesha mauaji ya watoto yaliyotokea mkoani Njombe. Amesema kuwa;
“Lengo la safari yetu ni kuja kuungana na kushirikiana na wataalamu wa mkoa wa Njombe kwa ajili ya kuona namna ya kuzuia au kuondokana na matatizo haya yanayojitokeza ya ukatili kwa kuwatumesikia mauaji yamejitokeza kwa mfululizo kwa hiyo kwa niaba ya katibu mkuu amenituma nitoe tamko la wizara kwa upande wa waganga wa jadi,anatoa wito kushirikiana katika kuwafichua waganga wenye kutoa masharti mabaya kwa wanaowahudumia kama wakatafute damu,viungo vya binadamu na kadhalika”
Aidha wizara hiyo imeomba vitendo vyote viovu na mifarakano miongoni mwa jamii vifichuliwe na kuchukuliwa hatua stahiki kwa wakati kutokana kuwepo njia mbali mbali za kufichua vitendo hivyo ikiwemo mamlaka za serikali za mitaa pamoja na jeshi la polisi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth msafiri amewata waganga hao wa tiba asili na tiba mbadala halmashauri ya mji wa njombe na wengine mkoani humo kufanya kazi kutokana na utaratibu waliopewa huku akiagiza kuondolewa kwa mabango yanayotangaza uganga bila utaratibu maalumu.
“Kuna vibao vya ajabu ajabu hapa na kama kuna watu wameweka vibao hapa muende mkaviondoe haraka sana, hakuna ruhusa ya kubandika kibao kama hakijapita sehemu husika,kama wewe unataka kujitangaza tukakuruhusu lakini tutafuata taratibu zote za tangazo maana vibao vingine ni vya uchonganishi”alisema Msafiri
Akizungumza kwa niaba ya waganga wengine wa tiba asili Dk.Mpapai,ameishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana na wataalamu hao huku akiomba kuendelea kupewa semina ya mara kwa mara ili kukumbushana.
“Jambo hili inatakiwa tuwe tunapewa semina ya mara kwa mara tunapata shida kwa kuwa hatuna elimu ya kutosha juu ya majukumu yetu sasa tunaweka maslahi mbele ya pesa bila kujua hatuna dawa bora sisi waganga tukiwa na dawa bora tutafanya biashara na tutapata pesa hakika haya matukio yametuumiza kweli kweli mpaka tumeanza kuishi kwa hofu na familia zetu”alisema Dk.Mpapai
Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Bw. Denis Bashaka amesisitiza suala la kujikita katika kufichua tatizo linalosababisha kutokea kwa mauaji hayo na kuangalia namna bora ya kuzifikia jamii kutoa elimu na kuzingatia Sheria, Sera na Miongozo katika kuandaa jumbe zitakazoweza kutoa elimu.
Aidha Wizara imekutana na Wataalam kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na Elimu mkoani Njombe kutengeneza jumbe maalaum zitakozotumika katika Jamii, Vyombo vya Habari katika kutoa elimu juu ya kuzingatia malezi bora kwa watoto na kuachana na mila zisizofaa hasa zinazoangamiza watoto.
Comments