Viwanja vya Mao Zedong Tung vyaleta faraja.

WADAU wa michezo Zanzibar wamepongeza hatua ya serikali kuvifungua viwanja vya  Mao Zedong  Tung kwa matumizi ya kawaida kwani kufanya hivyo kutaongeza ufanisi michezoni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Ali Abdulrahman, Hamza Ibrahim na Salma Sadik wachezaji na mashabiki walisema, hatua hiyo pia itasaidia kupunguza uhaba wa viwanja ambao ulikuwepo.
Walisema pamoja na ruhusa iliyotolewa ipo haja ya kuwekwa utaratibu na usimamizi madhubuti ili kulinda miundombinu iliyopo isiharibiwe.
“Mimi nadhani ipo haja ya kuwekwa usimamizi wa karibu utakaowawezesha wachezaji kutumia viwanja hivi kwa muda mrefu lakini pia uimara”, alisema Ali Abdulrahman.
Aliongeza kuwa uwanja unaotumika kwa mchezo wa mpira wa kikapu unaweza kutumika pia na michezo mingine kama vile mpira wa pete na mpira wa mikono, hivyo suali la usimamizi linapaswa kutiliwa maanani ili kuepusha migongano miongoni mwa wanamichezo hao.
“Mandhari ya uwanja yanamvutia kila mmoja hivyo suali la usimamizi uanzie na viongozi wa klabu, vyama vya michezo husika na hata wasimamizi wa uwanja kwani  serikali imewekeza fedha nyingi”, alisema Salma.
Hivi karibuni uwanja wa  Mao dze Tung  uliofanyiwa matengenezo makubwa na kuzindiliwa wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya mapinduzi mwezi Januari ulianza kutumiwa na wanamichezo wa michezo mbali mbali, ukiwemo soka ambapo michezo ya ligi juu ya Zanzibar ambayo awali ilipangwa kuchezwa saa nane zimeanza kuchezwa katika uwanja huo.
Zanzibarleo.

Comments