
Watu wasiojulikana katika shehia ya Uzi mkoa wa Kusini Unguja wamevamia matawi mawili na mabaraza matatu ya wanachama wa chama cha CUF na kuchana bendera usiku wa kuamkia jana.
Akithibitissha kutokea kwa tukio hilo mkurugenzi wa siasa na habari wa chama hicho jimbo la Tunguu, Juma Ali alisema haijajulikana nani amehusika na tukio hilo kwa vile limefanyika usiku wa manane.
Alisema matawi mawili na mabaraza matatu ya wanachama wa chama hicho milingoti ya bendera zake imekatwa na bendera kuchukuliwa na watu wasiofahamika.
“Kwa sasa tunajikusanya kwa ajili ya kwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi Tunguu ili waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria huku tukiamini kuwa waliofanya haya watadhibitiwa na kufikishwa kunakohusika,” alisema.
Baadhi ya wanachama wa CUF katika shehia hiyo walieleza kushangazwa na tukio hilo kwa vile wamekua wakifanya siasa kwa muda mrefu bila ya kugombana.
Mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama hicho, Salim Abdallah Bimani alipoulizwa alisema amepokea taarifa hizo na kwamba anashangazwa na tukio hilo ambalo anaamini lisingeweza kutokea wakati wa sasa.
Alisema kwamba tukio hilo si la kiungwana na kuwataka wanachama wa chama hicho kutokubali kuingizwa kwenye mitego ambayo alidai kuna watu wamedhamiria kufanya uchokozi ili utokee ugomvi ambao utakuwa na madhara makubwa kwao.
Comments