Oman yasema imeifungulia milango Zanzibar.

UBALOZI mdogo wa Oman uliopo Zanzibar, umesema daima milango yake iko wazi kusaidia upatikanaji fursa mbalimbali za mafunzo marefu na mafupi kwa watendaji wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
 Balozi mdogo wa taifa hilo Dk. Ahmad Hamood Al Habsi, ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) waliofika ofisini kwake Migombani kumshukuru baada ya kurejea kutoka Oman walikokwenda kwa ziara ya wiki mbili.
Dk. Al Habsi alieleza kuwa, ni wajibu wa Oman kuisaidia Zanzibar na wananchi wake, ambao kimsingi si marafiki wa nchi hiyo, bali ni ndugu wa damu wenye mafungamano ya kihistoria yanayowaweka pamoja.
Aliwataka wafanyakazi hao wayatumie mafunzo waliyopata wakiwa Oman katika kazi zao za kila siku kwenye mamlaka yao, ili yawe chachu ya mabadiliko na ufanisi katika shughuli za usafirishaji wa anga.
“Natumai ziara yenu Muscat haitakuwa ya matembezi tu, lakini mtaitumia kuwa ni darsa ya kujua namna bora ya kuipa hadhi mamlaka yenu kwa utendaji uliotukuka. Sisi tumetoa fursa mpira sasa uko kwenu,” alisema Balozi huyo.
Aidha aliwataka wawe mabalozi wazuri kwa wenzao ambao hawakupata fursa hiyo, kwa kuwaelekeza mambo mbalimbali waliyojifunza katika suala la usimamizi na uendeshaji wa shughuli za viwanja vya ndege.
Mapema, Mkurugenzi Viwanja katika Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar Zaina Iddi Mwalukuta, pamoja na kuushukuru ubalozi huo na serikali ya Oman kwa jumla, alisema ziara hiyo itasaidia kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Oman na Zanzibar.
Alishauri utaratibu huo uwe endelevu, ikizingatiwa Oman imepiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo, na kwamba Zanzibar inahitaji kuhimili kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya usafiri wa anga, utawala na ukarimu kwa wageni.
Naye Mkaguzi Mkuu wa hesabu za ndani katika mamlaka hiyo Safia Zubeir Abdulhamid aliyekuwa miongoni mwa wafanyakazi waliokwenda Oman, alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa kutokana na mambo waliyojifunza kila mmoja kwa idara yake.
Zanzibarleo.

Comments