Dk. Shein aahidi kutandika miundombinu Uzi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi, Dk.Ali Mohamed Shein, amesema  serikali itajenga daraja, barabara na skuli ya sekondari katika kijiji cha Uzi Ng’ambwa, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu  kwa wakaazi wa kijiji hicho na maeneo jirani.
Aliyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa skuli ya maandalizi na msingi katika kijiji hicho katika muendelezo wa ziara zake za kuangalia miradi ya maendeleo.
Alisema  barabara itajengwa kwa lami na itakuwa na urefu wa kilomita 7.5 itakayoanzia Unguja Ukuu hadi Uzi Ng’ambwa, sambamba na upatikanaji wa maji.
Alisema litajengwa tangi lenye uwezo wa kuchukua lita 5,000 na kwamba daraja litajengwa kutoka Unguja Ukuu hadi Uzi.
Alisema ujenzi wa daraja hilo utasaidia wananchi wa kisiwa hicho kuvuka bila kutegemea kujaa na kupwa kwa maji sambamba na kuongeza kazi ya utekelezaji wa  kasi ya kiuchumi.
Alisema serikali inaendelea kuwatumia wataalamu wake na washauri elekezi katika kufanya tafiti ili kuhakikisha miundombinu inajengwa kwa kiwango bora.
Alisema kijiji hicho ni maarufu ulimwenguni kote na wageni wengi hufika huko kukitembelea, hivyo serikali imedhamiria kwa dhati kukifikishia huduma muhimu za kijamii ili kiendelee kuwa kivutio.
Alisema serikali haitasita kuwashughulikia watu wanaosafirisha bidhaa kwa njia ya magendo hasa ikizingatiwa wanapunguza mapato ya serikali.
Alisema magendo yanaviza maendeleo na mipango ya serikali, hivyo  serikali itataifisha chombo kitachojihusisha na vitendo hivyo.
Alisema licha ya kuwepo sheria bado wapo watu wanaokwenda kinyume  na hatimae kuendeleza tabia ya kusafirisha bidhaa za magendo ikiwemo sukari, mchele, mafuta ya kupikia  kwa lengo la ukwepaji kodi.
Alipongeza juhudi zinazochukuliwa na kikosi cha kuzuia magendo kwa kazi kubwa ya kupambana na magendo kwa maslahi ya nchi.

Comments