
SERIKALI imesema bado ina fursa ya kukopesheka kwa vile ipo katika kiwango cha chini cha kupewa mkopo katika mabenki ya dunia.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Mohammed Salum, aliyasema hayo jana wakati akitoa majumuisho ya ripoti ya kamati ya kudumu ya bajeti ya baraza la wawakilishi kwa mwaka wa fedha 2018/2019, katika ukumbi wa baraza hilo, Chukwani.
Ripoti hiyo, iliyowasilishwa na Mwakilishi wa jimbo la Mpendae, Mohamed Saidi Dimwa, ilifahamisha kwamba deni la taifa hadi kufikia Febuari 2019, ni shilingi 444.480 bilioni linalojumuisha deni la ndani la shilingi 162.870 bilioni na deni la nje shilingi 281.601 bilioni.
Mwakilishi huyo ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema sababu za kuwepo kwa deni la ndani ni pamoja na kuongezeka kwa madeni ya wazabuni, mikopo, hati fungani na kuongezeka kwa madeni ya kiinua mgogo.
Upande wa deni la nje, Dimwa alisema limesababishwa na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.
Akitoa majibu ya taarifa hiyo, Dk. Khalid, alisema deni la Zanzibar lipo chini na bado serikali inaweza kukopa.
“Bado uwezo wa kukopa tunao na kama tungepata miradi hii tuliyopanga basi deni letu lingeongezeka na lingekuwa linalipika lakini tunakopa kwa miradi yenye tija,” alisema.
Alisema kuna baadhi ya nchi zimekopa kwa wastani wa asilimia 20 na yapo mataifa yamekopa kwa asilimia 40 hadi 45 ya pato lao la taifa, lakini Zanzibar bado ipo katika kiwango cha chini na deni lake linalipika.
Kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi, alisema, bado haikuwa ya kiwango cha kutisha kwani ilishuka kwa asilimia 1.5.3 ikiwa ni kiwango kidogo.
Akizungumzia bandari ya Mwangapwani, alisema wameanza kupeleka huduma muhimu zikiwemo za maji na barabara ikiwa ni hatua ya kuimarisha miundombinu ya maeneo hayo.
Alisema serikali inafanya mazungumzo na benki ya Exim ya Indonesia ili kupata mkopo nafuu utakaowezesha kutekeleza mradi huo.
Kwa ujenzi wa bandari ya Mpigaduri, alisema upo pale pale na unatarajiwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Comments