Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana Tarehe 10 Januari 2019
ameshuhudia hafla ya utiaji saini mikataba ya ubanguaji korosho kati ya
Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania na wenye viwanda vya
ndani.
Mkurugenzi
wa Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania Dkt Hussein Mansoor
ndiye ametia saini kwa niaba ya serikali na Kampuni nne zimesaini
mikataba ya awali kuanza kazi hiyo ambazo ni kampuni ya Hawte Investment
Co. Ltd, Micronix Mtwara, Korosho Afrika, na Micronix-Newala.
Kampuni
hizo zimeingia mikataba ya Jumla ya Tani 7500 ambapo kampuni ya Hawte
Investment Co. Ltd yenye uwezo wa kubangua Tani 2000 kwa mwaka imesaini
mkataba wa Tani 1500.
Kampuni
ya Micronix ya mjini Mtwara yenye uwezo wa kubangua Tani 2400 kwa mwaka
imeingia mkataba wa Tani 1200. Kampuni ya Korosho Afrika ya Mjini
Tunduru Mkaoni Ruvuma yenye uwezo wa kubangua Tani 5000 kwa mwaka
imeingia mkataba wa kubangua Tani 2400 ilihali Kampuni ya Micronix ya
Wilayani Newala yenye uwezo wa kubangu Tani 5000 kwa mwaka imeingia
mkataba wa kubangua Tani 2400.
Akizungumza
katika hafla hiyo ya utiaji saini Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga
(Mb) amesema kuwa serikali imepitia vifungu vyote vya kisheria kabla ya
kuanza kuingia makubaliano na kampuni hizo kwa ajili ya ubanguaji wa
Korosho.
Alisema
kuwa zoezi la ubanguaji tayari lilikuwa limeanza kupitia Shirika la
Kushughulikia viwanda vidogo vidogo (SIDO) ambalo tayari limeajiri
wafanyakazi 160.
Alisema
kuwa Shirika la Kushughulikia viwanda vidogo vidogo (SIDO) pamoja na
majukumu mengine lakini lilikuwa na kazi mbili ambazo ni kuhakikisha
wanatengeneza vipuli na mashine mbalimbali ambazo zimeharibika.
Vileviele kuhamasisha wabanguaji wadogo wadogo na kuwasajili.
“Baada
ya kuwasajili mtatakiwa kuingia nao mikataba kwa kiasi cha korosho
wanachokihitaji kwa ajili ya ubanguaji” Alikaririwa Mhe Hasunga
Mhe
Hasunga alisema kuwa serikali ina matumaini makubwa kuwa mikataba ya
ubanguaji iliyosainiwa itazingatiwa kwa kufuata taratibu na masharti
yote kwa mujibu wa sheria.
Alisisitiza
kuwa serikali inaingia mikataba na viwanda ambavyo vimekuwa vikibangua
kwa muda mrefu hivyo haina mashaka na ubora wa ubanguaji.
Aidha,
Alisema kuwa viwanda hivyo vitakuwa na uhakika wa kufanya kazi usiku na
mchana kutokana na malighafi nyingi iliyopo tofauti na miaka iliyopita
ambapo malighafi ilikuwa haipatikani kutokana na korosho kubanguliwa nje
ya nchi.
Mhe
Hasunga amesisitiza kuwa serikali imeamua kubangua korosho zote nchini
ili kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi sambamba na kuongeza thamani ya
korosho inayozalishwa nchini ili iweze kuuzwa kwa jina la Tanzania.
Ambapo Wizara ya Kilimo itaweza kuchangia kwa ufasaha katika uchumi wa
nchi.
Comments