Sherehe CCM kuadhimishwa kimkoa.

SHEREHE za miaka 42 ya kuzaliwa CCM, zitafanyika kila mkoa wa Tanzania, tofauti na miaka mingine ambapo maadhimisho ya kitaifa yalifanyika katika mkoa mmoja.
Hayo yalielezwa na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Kisiwandui.
Alisema kwenye sherehe hizo kutakuwa na uingizaji wa wanachama wapya watakaokuwa wamemaliza mafunzo katika darasa la itikadi.
“Sisi tunaenda sambamba na utekelezaji wa serikali kwani pesa ambazo zilitakiwa zitumike kufanya shughuli hii kitaifa basi zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo ya chama kimikoa,” alifafanua.
Aidha alifahamisha kuwa, kwa kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa Tanzania Bara, hivyo kauli mbiu ya mwaka huu inasema, tujipange kwa pamoja ili kuleta ufanisi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Alitoa wito kwa wanachama katika kuelekea uchaguzi mkuu wa taifa mwaka 2020, juu ya umuhimu wa kuwa na kadi ya kupigia kura.
“Wito wangu ni kwamba tunaelekea 2020, nataka kuona kila mwanaCCM anakuwa na kadi yake ya kupigia kura,” alisema.
Aidha alifahamisha kuwa, kwa wale wote ambao wataamua kujiunga na CCM kwa kipindi hiki cha miaka 42 ya chama hicho, basi milango ipo wazi.
Aidha aliwataka viongozi wa kila eneo kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ilani ya chama kwenye wadi, wilaya, majimbo na mikoa.
zANZIBARLEO.

Comments