Serikali Yatoa Bilioni 2.5 Kwa Ajili Ya Ujenzi Wa Jengo La Mama Na Mtoto Hospitali Ya Rufaa Ya Mkoa Wa Shinyanga.
Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.5 zitakazotumika katika ujenzi wa
jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga,
lengo likiwa ni kutoa huduma za kibingwa kwa akina mama wajawazito na
watoto wachanga.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea ujenzi wa Hospitali hiyo
na kukuta jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Utawala likiwa limekamilika.
Waziri
Ummy amesema fedha hizo zitafika katika Hospitali hiyo ndani ya wiki
mbili ili ziweze kuchochea kasi ya ujenzi na lengo ifikapo mwezi
Septemba 2019 Hospitali hiyo ianze kutoa huduma za afya.
“Ninaahidi
kutoa shilingi bilioni 2.5 ndani ya wiki mbili ziweze kutumika katika
ujenzi wa jengo la mama na mtoto, lengo la serikali ni kuhakikisha kila
mama mjamzito anapofika Hospitalini kujifungua atoke akiwa salama yeye
na kichanga chake”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri
Ummy amefikia uamuzi huo baada ya kupokea ripoti ya mkoa kuhusu vifo
vitokanavyo na uzazi kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Mfaume Rashid,
ambapo kwa mwaka 2016/2017 kulikua na vifo 73, na mwaka 2017/2018 vikiwa
ni vifo 56, hali ambayo Waziri huyo ameonekana kutoridhishwa nayo.
Hata
hivyo Waziri Ummy ameahidi kuongeza fedha zingine kiasi cha shilingi
bilioni 3 ndani ya mwezi mmoja, zitakazotumika katika ujenzi wa jengo
kwa ajili ya huduma za uchunguzi ikiwemo huduma za maabara, X-ray na
CT-Scan pia jengo hilo litakua na vyumba vitatu vya upasuaji.
Waziri
Ummy amesisitiza ujenzi wa jengo hilo utumike wa mfumo wa Force Account
ambao utahakikisha wananchi wanashiriki kwa asilimia 100 katika
kufanikisha ujenzi huo na huduma za afya zianze kutolewa mapema.
Wakati
huo huo, Waziri Ummy ametembelea kituo cha afya cha Kambarage katika
Manispaa ya Shinyanga kuona hali ya miundombinu ya kituo hicho na utoaji
wa huduma za afya huku kwa kiasi kikubwa akionekana kuridhishwa na kasi
ya ujenzi wa majengo ya huduma mbalimbali.
Kuhusu
uhaba wa watumishi wa kada za afya Waziri huyo ameahidi kutatua
changamoto hiyo hali inayopelekea kuwepo kwa msongamano wa wagonjwa.
Aidha,
Waziri Ummy amehitimisha ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa
kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kuridhishwa kwa
kiasi kikubwa na hali ya utoaji wa huduma za afya hasa katika jengo la
huduma za mama na mtoto na pia katika jengo la kuhifadhia watoto
wachanga wenye uhitaji wa uangalizi maalumu (NICU).
Mpekuzi.
Comments