Serikali imeagiza wavuvi waliokamatwa kwa kosa la kutohuisha leseni zao na vyombo vyao kwa mwaka 2019, waachiwe na makosa yao yafutwe mara moja.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Ulega alisema wizara juzi ilipata taarifa kutoka vyombo vya habari kwamba wavuvi katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi hususani soko la Feri, Dar es Saalam, hawakwenda kuvua samaki kwa sababu ya kutokuwa na leseni za vyombo vyao na za uvuvi kwa mwaka 2019.
Kutokana na hali hiyo, Ulega aliagiza wavuvi wote waliokamatwa kwa kosa hilo kote nchini, kuachiwa mara moja kuendelea na shughuli zao.
Pia aliwataka maofisa uvuvi kutoka katika ofisi zao na kuwafuata katika mialo mbalimbali ili kuwakatia leseni.
"Kwa kuzingatia kuwa hiki ni kipindi cha mwanzo wa mwaka na leseni zinatolewa, wizara inaelekeza kwamba wavuvi wote waendelee kukatiwa leseni hadi Januari 31,” alisema.
Aidha, aliagiza maofisa wote wa wizara na halmashauri katika kipindi hiki wawafuate wavuvi kwenye mialo ili kuwakatia leseni wenye sifa kulingana na sheria na kanuni za uvuvi.
Ulega alisema wizara inalo jukumu la kuhakikisha rasilimali za uvuvi nchini zinasimamiwa, kuhifadhiwa na kuvunwa kwa kuzingatia sheria ili ziwe endelevu.
"Kazi hii inapaswa kufanyika kwa kushirikiana na halmashauri nchini na wadau wa uvuvi,” alisema.
Aliongeza kuwa katika kutekeleza jukumu hilo wizara imekuwa ikiendesha operesheni dhidi ya uvuvi haramu na biashara haramu ya samaki na mazao yake kwa takribani mwaka mzima.
Comments