Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda Amuomba Msamaha Rais Magufuli.....Amtaka Awahurumie ili Nao Watoke Kifungoni.
Wakati
Rais John Magufuli akieleza sababu zinazomzuia kukutana na wanasiasa,
viongozi wa vyama vya upinzani wamemtaka asiwe na hofu kukutana nao na
kwamba pengine mtu aliyetishia kumchinja, alikuwa na maana ya “kuchinjwa
kisiasa”.
Akizungumzia
ushauri uliotolewa na Askofu Zachary Kakobe wa Kanisa la FGBF kutaka
wanasiasa wakutane kama walivyofanya viongozi wa kidini, Rais alisema
amekuwa akisita kwa sababu baadhi ya wanasiasa wanamtukana na wengine
wametishia kumchinja na kumtupa baharini ndio maana ameamua awaache peke
yao. Hata hivyo, alisema yuko tayari kukutana nao.
Hayo
yalitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati wa
mapokezi ya ndege mpya ya Serikali aina ya Airbus A220-300, ambako
viongozi kadhaa wa kidini walipewa nafasi ya kufanya sala, akiwemo
Askofu Kakobe, ambaye kabla ya sala aliomba aseme neno.
“Nimeusikia
wito wa Mzee Kakobe kuwa walipokutana na wao (viongozi wa dini) kule,
basi na sisi wanasiasa tuwe tunakutana,” alisema Rais.
“Mimi
nimekubali sana, lakini tatizo ni kuwa huwezi kukutana na mtu
anayekutana na kukuambia siku uchinjwe, utupwe baharini. Je, siku
ukikutana naye iwe ndiyo siku ya kuchinjwa?”
Kauli
hiyo ilimfanya mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda
aombe radhi kama kiongozi wa wadau wa siasa na kwa niaba ya vyama vyote
iwapo kuna kauli zimewahi kutolewa zenye mbomoko wa maadili.
“Nampongeza
kwa kutambulisha utashi wake wa kutaka kukutana na viongozi wa vyama
vya siasa. Hivyo kama kuna kauli ambayo imewahi kumkwaza atusamehe sisi
wadau wa siasa kama ambavyo amekuwa akisamehe wafungwa ili na sisi
tutoke kifungoni. Adhabu ya miaka mitatu inatosha,” alisema.
Alisema
Rais anapaswa kuwapangia fursa ya kukutana nao ili awaeleze hisia zake
na wao waeleze zao ili kudumisha utamaduni mzuri wa siasa kwa kuwa
Tanzania ina deni la kuwa kielelezo cha siasa bora ya demokrasia ya
vyama vingi.
Naye
mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia alisema
bado msimamo wake ni meza ya mazungumzo na kwamba hata alipokutana na
Rais Ikulu, Novemba 13 mwaka jana alimsisitiza jambo hilo.
“Kauli
ya mtu mmoja asiichukulie vibaya. Anatakiwa kujua kuwa yeye ni jalala,”
alisema mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi akirejea msemo maarufu wa
“ukubwa ni jalala”.
“Awe na moyo wa uvumilivu, aweke kipaumbele cha taifa mbele kwa kuwa nchi ni kubwa zaidi ya mtu yeyote.”
Alisema Watanzania wote wanapaswa kutunza nguzo ya hekima, umoja na amani kwa kuwa jamii yoyote yenye migogoro haiwezi kustawi.
Mbatia
alitoa mfano wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mpinzani wake mkuu,
Raila Odinga ambao siku za hivi karibuni walishikana mikono kumaliza
tofauti zao na wamekuwa wakionekana pamoja katika shughuli za kitaifa,
kijamii na kiserikali.
Mpekuzi.
Comments