Muarobaini kupunguza migogoro ya ndoa wapatikana.

WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, amesema serikali inaendelea kuchukua hatua kusimamia maslahi bora ya mtoto ikiwemo kutungwa kwa sheria ya watoto ya mwaka 2011, ambayo itawasaidia kupatikana kwa haki.
Hayo aliyasema wakati akifungua jengo la usuluhishi mahkama ya kadhi Mwanakwerekwe Unguja.
Alisema serikali imeanzisha sheria ya mahakama ya kadhi ambayo imepewa uwezo wa kusikiliza mashauri na matunzo, malezi ya watoto ili kuhakikisha wanapata haki zao.
Hata hivyo, alisema serikali hairidhishwi na ongezeko la migogoro ya ndoa, ndio sababu ikaanzisha mpango huo ili kupunguza tatizo hilo ambalo linaathiri malezi ya watoto.
Waziri Castico alifahamisha kuwa chanzo cha talaka nyingi kinatokana na umri mdogo wa ndoa pamoja na ukosefu wa elimu ya ndoa, hivyo kuathiri kizazi cha wanandoa na kuwakosesha haki zao.
“Serikali tayari imeshaleta muarubaini wa tatizo la migongano katika ndoa, pande mbili zinazozozana hufanyiwa suluhisho kabla ya mahakama, kwani naamini Masheikh waliobobea wapo wa kutosha wa kuyafanya hayo”, alisema Waziri Castico.
Castico alisema vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto vimeongezeka, matokeo yake husababisha watoto kubakwa, kutelekezwa na kunyimwa haki zao.
Alisema jitihada zinaendelea kuchukuliwa kuondosha changamoto za talaka kwa kudumisha upendo kwa jamii na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, alisema kufunguliwa kwa jengo hilo kutatoa fursa kwa wananchi ambao wana matatizo ya ndoa kupata fursa ya kusikilizwa na kupata suluhu.
Alisema chimbuko la kujengwa kwa jengo hilo kunatokana na ushawishi wa wizara ya kazi kwa kushirikiana na Save the children, katika kutekeleza sera ya kuwalinda wanawake na watoto ili kuepusha vitendo vya udhalilishaji.
Zanzibaleo.

Comments