Zikiwa
zimesalia siku nane kabla ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali
(CAG), Prof. Mussa Assad, kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa kwamba Bunge ni
dhaifu, Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika, naye amekoleza moto
kwa kusema Bunge la sasa ni dhaifu.
Mnyika
alitoa kauli hiyo jana wakati wa mjadala ulioshirikisha vyama vya siasa
kuhusu Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ulioandaliwa na Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ulioongozwa na Rais wa chama hicho,
Fatma Karume.
Alipoanza
kuchangia, Mnyika aliwashukuru TLS kwa kuandaa mjadala huo na kuahidi
kuwa maoni mbalimbali yaliyotolewa washiriki wa mkutano huo, Chadema
itayachukua kwa ajili ya kusukuma mabadiliko ili hatimaye wahakikishe
ile nia mbaya ya muswada huo haitimii.
“Nianze
kwa kuwaeleza waziwazi na kuwaomba sana kwamba kwa muundo wa Bunge letu
lilivyo sasa na kwa namna Bunge lilivyo dhaifu, tukifikiria kuwaachia
wabunge na kuwaachia mchakato wa kibunge uendelee mpaka mwisho
tukitarajia kwamba mambo mabovu yaliyoelezwa kwenye muswada
yatabadilika, tutakuwa tunafikiria vibaya,” alisema Mnyika.
Mnyika
aliwaomba washiriki wa mjadala huo wasiishie kutoa maoni yao hapo bali
washirikishe taasisi za kidini na za kiraia ziende kwa wingi mbele ya
Kamati Dodoma kufikisha ujumbe kwamba muswada huo usiende mbele ya Bunge
badala yake uondolewe kabisa.
Januari
7, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimtaka CAG afike mbele ya Kamati hiyo,
Januari 21 kujieleza kutokana na kauli yake aliyoitoa Marekani wakati
akihojiwa na redio moja nchini humo kuhusu Bunge linavyotekeleza
mapendekezo ya ripoti zake.
Mbali
na kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya Kamati, Ndugai pia alimtaka
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, kuripoti mbele ya kamati hiyo,
Januari 22, mwaka huu, kuthibitisha madai yake aliyoyatoa kupitia
mitandao ya kijamiii kuwa Bunge ni dhaifu.
Aidha,
Spika Ndugai aliongeza kuwa CAG na maofisa wake wanaingia kwenye Kamati
ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Spika
alifafanua kuwa ripoti hizo zikifika kwenye kamati hizo ambazo
zinaongozwa na upinzani, muda wote maofisa wa CAG wanakuwapo kueleza
upungufu waliobaini na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Ndugai
alisisitiza kuwa tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani,
imekuwa ikipambana dhidi ya matumizi mbaya ya fedha za umma na hatua
zimekuwa zikichukuliwa.
Kadhalika, Ndugai alibainisha Bunge
lilivyofanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka mitatu tangu serikali
ya Rais John Magufuli, ilipoingia madarakani mwaka 2015.
Ndugai
ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), alisema mabadiliko makubwa kwenye
usimamizi wa fedha za umma yamefanyika kwa ushauri wa Bunge na CAG,
hivyo alishangazwa na hatua zipi ambazo CAG alitaka zichukuliwe.
Mpekuzi.
Comments