MAVUNO ya mpunga katika bonde la Kibonongwa Donge Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, yanatarajiwa kuongezeka kutokana na upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati.
Wakulima wa bonde hilo walieleza hayo wakati wakizungumza na gazeti hili jana.
Walisema zoezi la ulimaji na upandaji limeanza kwa wakati kutokana na juhudi na ushirikiano wa karibu kati yao na viongozi wa jimbo.
Mkulima Jabiri Khamis, alisema katika hatua ya awali zaidi ya hekta 80 zilizomo ndani ya bonde hilo zimelimwa na kupandwa mpunga.
Alitaja miongoni mwa mbegu wanazotumia ni pamoja na supa, india na nanenane, ambazo wanatarajia kutoa mavuno mengi.
Alisema kutokana na mavuno mazuri waliyoyapata msimu uliopita, umesaidia kuibua ari na hamasa kwa wakulima.
Pamoja na mafanikio hayo, alisema bado wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mbolea, hivyo akawaomba viongozi wa jimbo kusaidia kulitatua tatizo hilo.
“Ingekuwa huduma za mbolea tunazipata kwa wakati kama tunavyopata huduma ya matrekta, naamini uzalishaji ungekuwa bora mara dufu,” alisema.
Nae mkulima Mkasi Juma, alisema vijana wengi wana mwamko wa kushiriki katika shughuli za kilimo jimboni humo hasa katika mazao ya kilimo cha biashara kama vile matango, mananasi, tungule na mahindi.
Zanzibarleo.
Comments