Jamii yahimizwa kuwatunza watoto.

JAMII imetakiwa kuzingatia malezi ya watoto wao ili kupunguza idadi ya watoto wanaotunzwa katika vituo vya kulelea watoto.
Mkurugenzi wazee na ustawi wa jamii, Wahida Maabadi Mohammed, alisema hayo katika ofisi ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Tunguu wilaya ya kati Unguja.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia watoto hao kulelewa katika mazingira bora kwa kuzingatia mila, silka na tamaduni za kizanzibari.
Alisema baadhi ya jamii zinakwepa majukumu ya malezi ya watoto wao na badala yake wanawapeleka katika vituo hivyo.
Akiwasilisha mada juu ya vyombo vya habari na malezi mbadala, Meneja utetezi wa TAMWA, Hawra Shamte, alisema vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuielimisha jamii juu ya malezi bora kwa watoto ili kuwajenga katika maadili mazuri.
Alisema vipo baadhi ya vyombo vya habari vinaandika habari za udaku na zisizo na maadili hali ambayo inasababisha kuipotosha jamii.
Alifahamisha kwamba vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwa jamii hivyo ni muhimu kutumika ipasavyo katika kuifahamisha jamii juu ya maovu yanayowakabili watoto wanaolelewa katika vituo.
Zanzibarleo.

Comments