Dk. Shein: Tutaimarisha huduma za uokozi.

 wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali itaendelea kuweka vifaa vya kisasa vya uzamiaji na uokozi kwa kikosi cha KMKM, ili kukabiliana na ajali zinazotokea baharini.
Alisema hayo, baada ya kuzindua boti ya uokozi na kituo cha uzamiaji na uokozi kinachomilikiwa na KMKM kilichopo bandarini Mkoani Pemba, ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za miaka 55 ya mapinduzi Zanzibar ya 1964.
Alisema, baada ya Zanzibar kukumbwa na majanga ya baharini mwaka 2011 na 2012, serikali ikadhamiria kutafuta mradi mkubwa kwa lengo la kununua vifaa vya kisasa vya uokozi, ili kukabiliana na ajali za majini.
Alisema ununuzi wa vifaa hivyo, ikiwemo boti zenye vifaa vya kisasa ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, sambamba na utekelezaji wa azma ya mapinduzi.
Alisema, serikali inataka kuona kila mwananchi anaishi kwa usalama na amani hata akiamua kusafiri iwe nchi kavu, baharini au angani.
Alisema serikali, inataka kuona usafiri wa aina zote unaimarika, ndio sababu inatumia fedha nyingi kuhakikisha kunakuwa na usafiri wa uhakika.
“Ndio maana tumeamua kuwa na mradi huu wa Zanzibar salama, ambao unahusisha ujenzi wa vituo sita vya uokozi, ununuzi wa boti za uokozi, mafunzo kwa askari, wananchi na vifaa vya kisasa ili usalama upatikane,” alieleza.
Alisema serikali ililamizika mwaka 2013/2014 kubuni mradi wa Zanzibar salama na utekelezaji wake ukaanza 2015 kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na uokozi wa uhakika na wa kisasa.
“Kila mmoja ni shahidi kuwa tulipata misiba ya Mv Spice Islander na Skagit sasa kwa matukio hayo, tulipata funzo pale tulipokosa namna ya kuwaokoa wenzetu waliozama, lakini sasa tumepata vifaa vya kisasa,” alieleza.
Alisema pamoja na kuwepo boti na vifaa vya kisasa vya uokozi, serikali pia inayo meli ya kuzimia moto baharini, ambapo yote hayo ni kuhakikisha wananchi wanaotumia usafiri wa bahari, wanakuwa salama.
Alisema zipo boti nyengine ndogo ndogo zenye mwendo kasi, ambapo zote hizo ni sehemu ya mradi huo.
“Naomba wananchi niwambie kuwa, serikali yetu imejipanga vya kutosha tena kwa kuwa na vifaa vya kisasa, na wazamiaji watakuwa na boti yao maalumu ambayo inatarajiwa kuwasili mwezi huu,” alisema.
Aliongeza kuwa, sehemu ya pili ya mradi huo mkubwa ni uwekaji wa kamera za kutunza usalama CCTV ambapo kwa sasa katika eneo la Mji Mkongwe pekee zimefungwa 687, mbali na maeneo mengine ya Unguja.
“Kwanza tumeanza kwa Mji Mkongwe na miji mengine ikiwemo minne ya Pemba, itawekewa kamera hizo endapo uchumi utaruhusu hapo baadae,” alieleza.
Kuhusu uwepo wa vikosi vya JKU, KMKM, KZU, KVZ na Chuo cha Mafunzo Zanzibar, alisema vikosi vipo kwa mujibu wa katiba na sheria za Zanzibar na wala haviendeshwi kwa matakwa ya mtu.
Alisema cha mwanzo kilichoanzishwa kilikuwa ni KMKM wakati huo wakiitwa wanamaji, na haviendeshwi kama wanavyotaka wao, bali ni kwa mujibu wa sheria.
“Wale wanaodhani kuwa vikosi hivyo vipo kwa bahati mbaya na vinajiendesha vipendavyo, sio sahihi bali wanakwenda kwa mujibu wa sheria wala havishirikiani na wanaoharibu amani na utulivu,” alieleza.
Awali akisoma taarifa ya kiufundi Mkuu wa KMKM Zanzibar, Hassan Mussa Mzee, alisema ujenzi wa vituo vya uzamiaji wa uokozi Zanzibar, unagusa moja kwa moja maisha ya wananchi wote wa Zanzibar.
Alisema mradi huo, umejumuisha majengo, ununuzi wa boti za uokozi na vifaa mbali mbali vya kisasa vya uokozi na vya mawasiliano.
Alisema kati ya vituo hivyo sita, vilivyokamilika ni vitatu ambavyo ni Kibweni, Nungwi na Mkoani, ambapo kila kituo kinatarajiwa kuwa na boti za wazamiaji, vifaa na mitambo kwa ajili ya kazi ya uokozi.
Katika hatua nyengine, alisema mradi huo ni utekelezaji kwa vitendo wa malengo ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambapo kwa mwaka huu yanatimiza miaka 55.
“Tunaahidi kuwa majengo, vifaa na boti tutavitunza na kuvilinda kwa nguvu zetu zote, ili kuhakikisha mradi huo mkubwa unafikia malengo yaliokusudiwa ambayo ni kuwaokoa wananchi wetu,” alifafanua.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa, Idara Maalum za SMZ, Radhia Rashid Haroub, alisema mradi huo ulitengewa shilingi bilioni 5.9 hadi kumalizika kwake, ingawa gharama ziliongezeka kutokana na mahitaji na ongezeko la thamani vya vifaa.
Alieleza kuwa, mradi huo una maeneo makuu manne, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo sita vya uokozi, kununua boti na vifaa vyake, kununua vifaa vya mawasiliano na mafunzo kwa askari na wananchi.
Alieleza kuwa, vituo viwili vilivyokamilika vya Kibweni na Mkoani Pemba, vimegharimu shilingi milioni 966.8.
“Aidha ununuzi wa boti mbili za uokozi, serikali imegharimu shilingi bilioni 12.5, ambapo pia kuna ununuzi wa nguo za uokozi, mitungi ya gesi, mashine ya kutengenezea gesi na vifaa wakati wa uokozi chini ya bahari ambapo vimegharimu shilingi milioni 500,” alifafanua.
Awali Dk. Shein, alizindua boti za uokozi kwa kituo cha KMKM Mkoani na kisha kukifungua kituo kipya cha uokozi bandarini hapo.
Shamra shamra shamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizinduliwa Disemba 31 mwaka jana, kwa kazi za usafi wilaya zote za Unguja na Pemba, ambapo kilele chake kinatarajiwa kufanyika uwanja wa Gombani, Januari 12.

Comments